Nawanda afunguka magumu aliyopitia katika kesi ya ulawiti

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 11:51 AM Dec 31 2024
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda.
Picha:Mtandao
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda.

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda amezungumza kwa mara nyingine baada ya kushinda kesi ya ulawiti, akisimulia magumu aliyopitia kipindi chote cha kesi hiyo.

Dk. Nawanda alieleza hayo juzi wakati wa misa ya kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan na kumkumbuka baba mzazi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa iliyofanyika katika mtaa wa Nyakabindi, mjini Bariadi.

Alisema kuwa kipindi cha kesi yake kilimfundisha thamani ya kuishi vizuri na watu, akitoa shukrani kwa wananchi wa Simiyu kwa madai walionesha mapenzi makubwa na walimwombea kwa bidii.

"Niwashukuru wananchi kwa dua na maombi yenu ambayo mlikuwa mkiniombea wakati ninapitia kipindi kigumu sana ambacho pia nilihitaji uwapo wa Mungu. Kwa hakika Mungu anampa mtihani mtu anayempenda," alisema Dk. Nawanda.

Alisema kuwa wakati wowote Mungu hawezi kumpa mtihani mja wake ambao hawezi kuuhimili na kuwa alipewa mtihani huo akijua kuwa atauhimili.

"Pia alijua nina watu na watu ndiyo ninyi. Kwahiyo jamani ninawashukuru sana kwa dua zenu. Ninawashukuru kwa kila kitu," alisema Dk. Nawanda.

Aliwashauri viongozi kuishi vizuri na watu na kwa ukaribu kwa kuwa hakuna anayetambua kesho yake. Alisema ukaribu huo ni watu ni mtaji mkubwa katika maisha yake.

"Mwaka jana nilikuja hapa kama mkuu wenu wa mkoa lakini mwaka huu nimekuja kama Nawanda tu wa kawaida. Kwahiyo Simalenga (Mkuu wa Wilaya ya Bariadi) haya maisha yanabadilika sana," alisema Dk. Nawanda.

Alisema kuwa sasa ameamua kuwekeza nguvu zake Newala na kuwa anapambana kwa ajili ya eneo hilo, akitaja kuwa na jambo lake aliloliacha katika kile alichokiita "mabano na litajulikana rasmi 2025".

"Hata hivyo, hili jambo langu la Newala limeishaisha, hivyo msiniulize ni jambo gani, nitawaambia mwakani na wakati utakapofika 2025," alisema Dk. Nawanda.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema ni muhimu kumwombea Rais Samia kutokana na kazi anayofanya katika kuletea taifa maendeleo.

Novemba 20 mwaka huu, Dk. Nawanda aliachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza baada ya kutomkuta na hatia katika kesi ya kulawiti iliyokuwa inamkabili.

Dk. Nawanda alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Julai 9, 2024 na kusomewa shtaka moja la kulawiti kinyume cha kifungu namba 154 (1)(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, SURA 16, kosa alilodaiwa kutenda Juni 2, 2024.

Alidaiwa kumlawiti mwanafunzi wa chuo kimoja mkoani Mwanza katika eneo la maegesho ya magari lililoko Rock City Mall, wilayani Ilemela mkoani hapa.