WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaongoza viongozi na wananchi katika mazishi ya Jaji Fredrick Werema, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akimwagia sifa kuu tano za kisheria na uongozi.
"Alikuwa mtu mwenye msimamo, akiamini kitu anafanya na kutenda vilevile. Hakuwa na lugha za kuchanganya, alikuwa mwadilifu na alitumikia taifa kwa uwezo wake wote," Jaji Warioba amesema.
Ilikuwa katika tukio la kuaga mwili wa Jaji Werema kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana.
Warioba alisema kuwa Jaji Werema atakumbukwa kwa mengi katika utumishi wake wa umma.
Wasifu huo uliendana na kilichoelezwa na aliyemteua katika nafasi ya kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2014, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.
Mkuu huyo wa nchi mstaafu alimwelezea Jaji Werema kuwa mwanasheria mbobevu; mzalendo wa dhati na mara zote alitoa ushauri makini uliozingatia maslahi ya taifa huku akimtaja kuwa mahiri na mpenda haki.
"Amefanya mengi mema kwa taifa na ameacha alama ya kudumu nchini. Nilimteua kuwa jaji kutokana na sifa zake katika utendaji," Kikwete alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa katika tukio hilo, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, alieleza masikitiko ya Mkuu wa Nchi wa sasa aliyemworodheshea wasifu wa Jaji Werema kuwa kiongozi shupavu, aliyekuwa mwadilifu na mwenye msimamo wakati wote wa utendaji kazi wake.
"Mheshimiwa Rais anajua kwamba Jaji Werema alifanya kazi katika mihimili yote na ana uzoefu mkubwa wa utendaji katika mihimili yote, mengi mazuri ameyatenda.
"Rais Samia anawasihi wote muwe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu na ametusihi tuendelee kumwombea na kuenzi yote aliyoyafanya katika utumishi wake," alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa huyo kuwataka wanasheria na watanzania kwa ujumla kuenzi na kuendeleza yale yote mazuri aliyofanya Jaji Werema enzi za uhai wake.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari alisema kuwa Jaji Werema alikuwa mtu mwenye maono na mtaalam wa sheria aliyejitolea na kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha sheria na haki zinatumika katika kuleta maendeleo kwa taifa.
"Jaji Werema alifanya maboresho makubwa katika mfumo wa sheria na haki na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha na kuimarisha utawala wa sheria na kuwaendeleza, kuwafunda na kuwanyanyua wanasheria waliokuwa wanachipukia, alionesha uongozi wa aina yake katika nyakati ngumu pia aliweza kupigania maslahi ya taifa," alisema.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Ally Possi alisema kuwa Jaji Werema alikuwa mahiri na nguzo imara katika sekta ya sheria nchini kwa kuwa aliendelea kutoa huduma katika sekta ya sheria hata baada ya kumaliza muda wake wa utumishi serikalini.
"Uimara wake katika maeneo mbalimbali ya sheria na uchapakazi wake vimeacha alama katika sekta ya sheria nchini," Dk. Possi alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED