HUKU ikiwa inahitaji pointi tatu muhimu kuweka hai matumaini yao ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga jana iliisambazia 'Gusa, achia, tende kwao' TP Mazembe na kuifumua mabao 3-1 kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ushindi huo sasa umeifanya Yanga kufikisha pointi nne na kupanda mpaka nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi A na kuiacha TP Mazembe ikiburuza mkia kwa pointi zake mbili huku Al Hilal ikiongoza kundi kwa pointi tisa na kufuatiwa na MC Alger wenye pointi nne sawa na Yanga lakini leo watakabiliana na vinara kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo.
Katika mchezo wa jana uliokuwa na mvuto, mabao mawili ya Clement Mzize na kiungo mshambuliaji Stephan Aziz Ki yalitosha kufifisha matumaini ya Mazembe kucheza hatua ya robo fainali.
Matokeo ya jana yalikuwa kama marudio ya kile kilichotokea, Februari 19, 2023, Yanga ilipoifunga timu hiyo idadi kama hiyo ya mabao kwenye uwanja huo huo katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Jana TP Mazembe ndio walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 15 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na golikipa wake Aliou Badara Fatty.
Kipa huyo raia wa Senegal, aliamua kwenda mwenyewe kupachika mpira wavuni, baada ya kutokea adhabu hiyo kubwa iliyotokana na Shadrack Boka, kumkwatua beki wa kulia wa Mazembe, Ibrahim Keita ndani ya eneo la hatari.
Bao hilo lilionekana kuwaamsha Yanga, ambao waliamua kuliandama kama nyuki lango la wapinzani wao, huku wakikosa mabao ya wazi kila wanapofika langoni.
Dakika ya 20, wachezaji wa Yanga waligongeana mpira vizuri lakini mpira wa mwisho ulimkuta Aziz Ki, lakini alipiga nje.
Alikuwa Mzize aliyewainua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kupachika bao la kusawazisha dakika ya 32 kwa shuti kali la mbali.
Baada ya TP Mazembe kufanya shambulizi, Yanga ilijibu kwa kuanzisha mpira haraka na kupasiana kwa haraka kabla ya mpira kumfikia Mzize aliyeachia shuti kali la juu, mpira ukamshinda kipa, Fatty na kujaa wavuni.
Kipindi cha kwanza kama Yanga ingekuwa makini ingeweza kupata walau mabao manne, kwani baada ya kufungwa bao hilo, wachezaji wa TP Mazembe walionekana kuchanganyikiwa na kutoa mianya kwa wapinzani wao ambao walifanya mashambulizi ya hatari, dakika ya 34 na 37 kupitia kwa Aziz Ki na Pacome, lakini hawakuwa makini kukwamisha mipira wavuni.
Hatimaye, Aziz Ki, alisawazisha makosa yake ya kukosa mabao mara kwa mara alipopachika bao maridadi dakika ya 56, kwa kumpiga tobo kipa Fatty.
Boaz Ngalamulume alirudisha mpira nyuma ambao ulinaswa na wachezaji wa Yanga na kupasiwa Khalid Aucho aliyempenyezea Aziz Ki ambaye alimfunga kwa tobo Fatty na kuiandikia Yanga bao la pili.
Dakika tatu baadaye, Mzize kwa mara nyingine alifunga bao lingine, likiwa la tatu kwa Yanga baada ya kuwazidi mbio mabeki wa TP Mazembe kabla ya kubaki na kipa na kuupeleka mpira upande wa kushoto wa golikipa na mpira kujaa nyavuni.
Kipigo hicho rasmi kimefuta matumaini ya TP Mazembe kutinga hatua ya robo fainali msimu huu kwani nayo ilikuwa ikihitaji ushindi kufufua matumaini yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED