JESHI la Polisi limekusanya zaidi ya Sh. bilioni 3.4 kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji sheria za usalama barabarani mkoani Mbeya katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga alisema makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la Sh. milioni 104.8 kulinganisha na makusanyo ya mwaka 2023 ambao walikusanya Sh. bilioni 3.3.
Kamanda Kuzaga alisema makusanyo hayo yamepatikana kutokana na makosa 115,216 ya ukiukwaji sheria za usalama barabarani yaliyoripotiwa mwaka 2024, yakiwa yamepungua kwa makosa 604 kulinganisha na mwaka 2023 ambao ulikuwa na makosa 115,820 yaliyorekodiwa.
Katika taarifa hiyo, Kamanda Kuzaga alisema madereva 28 walifungiwa leseni kwa makosa hatarishi ya usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na mwendo kasi, kuyapita magari mengine kwenye maeneo hatari na kusababisha ajali za vifo na majeruhi. Madereva 29 walifikishwa mahakamani kwa ukiukwaji sheria hizo.
Kamanda Kuzaga alitaja mafanikio mengine ya kiusalama mwaka 2024, akisema kuwa watuhumiwa 9,985 walikamatwa kwa makosa mbalimbali ya jinai na kufikishwa mahakamani.
Alisema kuwa jumla ya makosa ya jinai yaliyoripotiwa mwaka 2024 ni 22,049, yakiwa yamepungua kwa makosa 1,705 kulinganishwa na mwaka 2023 ambao ulikuwa na makosa 23,754 yaliyoripotiwa.
Kamanda Kuzaga pia alisema walikamata madini aina ya dhahabu yenye uzito wa kilogramu tisa na gram 622.76, yenye thamani ya Sh. bilioni 1.5.
Alisema madini hayo yalipatikana baada ya watuhumiwa sita kukamatwa. Nyara za serikali zenye thamani ya Sh. bilioni 288.9 zilikamatwa na watuhumiwa 31 walikamatwa (wanaume 29 na wanawake wawili).
Kamanda Kuzaga pia alieleza kuwa wahamiaji haramu 60 walikamatwa kutoka katika nchi za Ethiopia (43), Malawi (15), Burundi (1) na Rwanda (1). Silaha 12 na risasi 63 pamoja na baruti kwenye makopo madogo matatu zilikamatwa katika msako wa kiusalama.
Kamanda Kuzaga alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama katika kubaini na kuzuia uhalifu kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu, ili hatua stahiki zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa wahusika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED