NURU AWADH: Mwenyekiti mpya wa mtaa aliyeshinda vikwazo vya mfumo dume katika siasa

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:18 AM Jan 03 2025
Nuru Awadh, Mwenyekiti mpya wa mtaa wa Miembesaba B, kata ya Kongowe wilayani Kibaha.
Picha:Julieth Mkireri
Nuru Awadh, Mwenyekiti mpya wa mtaa wa Miembesaba B, kata ya Kongowe wilayani Kibaha.

"SIKU ya pili baada ya kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), niliumwa sana! Kila aliyekuja kuniona, aliniambia niachie hii nafasi mwanamume aingie kufanya kampeni maana huu ugonjwa ninaoumwa si hali ya kawaida," anaeleza Nuru Awadh, Mwenyekiti mpya wa mtaa wa Miembesaba B, kata ya Kongowe wilayani Kibaha.

Nuru (33) anasimulia kuwa haikuwa kazi rahisi kwake kumshawishi kila mtu ili amwelewe, lakini akashikilia msimamo wake wa kuendelea na matibabu huku akisubiri ufike muda wa kampeni nafasi yake Mwenyekiti Mtaa wa Miembesaba B.

"Niligombea kura za maoni tukiwa wanawake wawili na wanaume watano. Nilikatishwa tamaa na wengi, wakidai mimi mwanamke siwezi kuongoza wanaume, lakini nikapuuza maneno yao, wengine walisema nina asili ya kiarabu, sikukata tamaa," anasimulia.

Nuru ambaye aliongoza kwenye kura za maoni CCM kwa kupata kura 139, akifuatiwa na mtiania mwanaume aliyepata kura 113, alipogombea na vyama vingine kuwania nafasi hiyo, akatangazwa mshindi kuwa mwenyekiti wa mtaa huo.

"Baada ya ushindi ndani ya chama changu, uchaguzi ambao ulifanyika Oktoba 23, nilifuatwa nikitakiwa kuachia nafasi kwa mitazamo ya kuwa mtaa huo haustahili kuongozwa na mwanamke.

"Wakati ninaumwa kwa wiki nzima, nilikuwa sina uwezo wa kutoka ndani, hakuna mtiania mwenzangu ndani ya chama aliyefika kunijulia hali na hata wananchi waliofika, wimbo ulikuwa mmoja wakihusisha ugonjwa wangu na mambo ya ushirikina baada ya kuongoza kwenye kura," anasimulia.  

WAKATI WA KAMPENI

Nuru anaeleza kuwa wakati wa kampeni alipata nafuu ya maradhi yaliyokuwa yanamsibu, akifanya kampeni kwa kushirikiana na wanachama na viongozi wake wa mtaa na kata ya Kongowe kuomba kura.

Katika kampeni zake, mama huyo wa watoto watatu ambaye awamu iliyopita alikuwa mjumbe wa serikali ya mtaa huo, alinadi sera zake, akiahidi kutatua kero alizozitaja kuwa kikwazo kwa wananchi kufanya shughuli zao.

Anasema uhitaji wa zahanati, barabara na ofisi ya mtaa ni vitu ambavyo alisisitiza zaidi kwa wananchi, akiwaomba wamchague ili ashirikiane na viongozi wengine kupata majawabu.

"Mtaa wetu hauna zahanati, nitashirikiana na wananchi tujenge ili wasitumie gharama kwenda kufuata huduma za afya mbali na wanapoishi.

"Nitashirikiana pia na viongozi wangu, akiwamo diwani wa Kongowe kufuatilia kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) barabara yetu ifanyiwe ukarabati iweze kupitika wakati wote.

"Kitu kingine kilichonipa ushindi ni kunadi kwa wananchi kusudi langu la kujenga ofisi ya mtaa ambayo itarahisisha utoaji huduma kwa wananchi ambao kwa sasa wanatumia ofisi ya ofisa tarafa.

"Mtaa wetu hauna ofisi na mimi nitafanya kazi chini ya mkorosho kutoa huduma kwa wananchi. Tutaweka meza na viti nje. Kwa kufanya hivi, msukumo utakuwapo kwa wananchi kuchangia ujenzi wa ofisi yao na tutakapoishia tutaomba msaada kwa serikali itusaidie kumalizia," anasema.

BAADA YA UCHAGUZI

Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 zilifikia tamati Novemba 26 na uchaguzi wenyewe ukafanyika Novemba 27, Nuru akiwa tayari ameshazunguka katika kaya 1,655 na kufanya mikutano, akiomba wananchi wake wamchague kuongoza mtaa huo.

Nuru aliibuka mshindi na kutangazwa kuwa mwenyekiti baada ya kupata kura 927 akimshinda mpinzani wake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye alipata kura 191.

Anasema haikuwa kazi rahisi kupata nafasi hiyo kwa kuwa walio wengi walikuwa wakimkatisha tamaa kuwa hawezi kupata nafasi hiyo kwa kuwa ni mwanamke na mwenye asili ya kiarabu, hivyo hawezi kukubalika kwa wenyeji wa mtaa huo.

Akizungumzia ushindi wake, Nuru anasema vipaumbele vyake alivyonadi kwa wananchi ndivyo vilivyompata nafasi hiyo, pia ujasiri na kutokata tamaa.

"Vikwazo kisiasa kwa wanawake ni vingi ambavyo vikimkuta mtu ambaye hana uvumilivu, anaweza kujitoa kwenye nafasi anayogombea.

"Wanawake wanatakiwa kuondokana na dhana ya woga wa kugombea nafasi za uongozi kwa kuhofia ukabila, udini na imani za ushirikina. Kwa kufanya hivi tutakuwa na viongozi wengi katika ngazi tofauti," anasema Nuru.

Mwenyekiti huyo wa Mtaa wa Miembesaba B pia anawashauri wanawake ambao ni viongozi, wawe mashuhuda kwa wengine ili kuwapa ujasiri wa kugombea na kuwaondolea woga uliojengeka miongoni mwao, hata unawafanya washindwe kuingia katika uongozi.

Katika harakati zote hizo, Nuru anasema mumewe pia amekuwa anampa ushirikiano kuanzia alipochukua fomu hadi sasa.

WADAU WALONGA

Mwandishi wa makala hii alifuatilia kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024. Akifungua kampeni hizo, Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylvestry Koka alimzungumzia Nuru, akimpongeza kwa uchapakazi wake akiwa mjumbe wa serikali ya mtaa.

"Nuru ni mpambanaji, sina shaka naye na kila alichoahidi kwenye eneo lake tutashirikiana viongozi kutekeleza, hakuna kitu kinashindikana kwa serikali hii inayoongozwa na mama na hapa tunakwenda kumchagua mama," alisema.

Diwani wa Kongowe, Hamis Shomari, akiwazungumzia wanawake waliogombea na kupata nafasi katika kata hiyo, anasema kutokana na uzoefu walionao wenyeviti hao, hana shaka na utekelezaji ahadi walizotoa.

Shomari anasema kuwa kati ya mitaa sita ya kata hiyo, mitatu hivi sasa inaongozwa na wenyeviti wanawake ambao ni pamoja na Nuru Awadh (Miembesaba B), Mboni Mkomwa (Bamba) pamoja na Maimuna Sultani (Kongowe).

Anabainisha kuwa kabla ya uchaguzi huo, Nuru na Mboni walikuwa wajumbe wa serikali za mitaa yao huku Maimuna ambaye amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa mtaa huo kwa kipindi cha tatu.