Mauaji kigogo CCM: Mwenyekiti Wazazi, wenzao watatu kizimbani

By Francis Godwin , Nipashe
Published at 10:19 AM Jan 03 2025
Washtakiwa katika kesi ya jinai namba 34404 ya mwaka 2024 ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki wakitolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Iringa baada ya kesi hiyo kuahirishwa hadi Januari 7 mwaka huu.
Picha: Picha: Francis Godwin
Washtakiwa katika kesi ya jinai namba 34404 ya mwaka 2024 ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki wakitolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Iringa baada ya kesi hiyo kuahirishwa hadi Januari 7 mwaka huu.

WATU watano wamefikishwa mahakamani wilayani Iringa kwa mashtaka ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki.

Miongoni mwa washtakiwa hao, wamo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Kilolo, Hedikosi Kimwaga na Diwani wa Nyanzwa, wilayani Kilolo, Boniphace Katili.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani jana saa nane mchana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Rehema Mayagilo huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika viwanja vya mahakama hiyo.

Akisoma hati ya mashtaka katika kesi hiyo ya jinai namba 34404 ya mwaka 2024 ya mashtaka ya mauaji, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Sauli Makori alidai mahakamani huko kuwa washtakiwa hao; Kefa Wales, Silla Kimwaga, Boniphace Katili, Willy Chikweo na Hedikosi Kimwaga, kwa pamoja wanashtakiwa kumuua Christina Kibiki.

Alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo la mauaji Novemba 12, 2024 katika kijiji cha Ugwachanya, wilayani Iringa.

Hata hivyo, Makori alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Januari 7 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.