Shehena miundombinu ya serikali Iliyoibiwa Pwani yakamatwa

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:32 PM Jan 02 2025
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.

Serikali mkoani Pwani imekamata shehena ya miundombinu mbalimbali ya serikali iliyoibiwa na kuhifadhiwa katika kiwanda cha kutengeneza vifaa vya ujenzi cha LN Features kilichopo Mkuranga.

Hatua hiyo imefanikishwa na kikosi kazi maalum kilichoundwa na mkoa huo kwa lengo la kufuatilia uharibifu wa miundombinu kwenye taasisi mbalimbali, ikiwemo TANESCO, DAWASA, na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameongozana na viongozi wa Mkoa na Wilaya ya Mkuranga kukagua miundombinu hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari, Kunenge amesema baadhi ya wananchi wanahujumu juhudi za serikali za kuboresha huduma kwa kuiba miundombinu muhimu.

“Serikali imekuwa ikiboresha miundombinu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, lakini wapo wachache wanaoiharibu na kurudisha nyuma jitihada hizi. Hatutavumilia yeyote anayehusika,” amesema Kunenge.

Kunenge amesisitiza kuwa, pamoja na Mkoa wa Pwani kuongoza kwa uwekezaji wa viwanda, hawataruhusu wawekezaji wanaoshiriki kurudisha nyuma maendeleo ya taifa kwa kuhujumu miundombinu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Protus Mutayoba, amebainisha kuwa miundombinu hiyo imekuwa ikiibiwa kutoka maeneo mbalimbali na kupelekwa katika kiwanda hicho. Amesisitiza umuhimu wa oparesheni kama hiyo kufanyika katika maeneo mengine ili kukomesha biashara haramu ya miundombinu.

Meneja wa Huduma za Usalama wa TANESCO, Lenin Kiobya, ameeleza kuwa biashara ya kopa imechangia uharibifu mkubwa wa miundombinu ya umeme. Kwa kipindi cha Juni hadi Desemba 2023, transfoma 33 ziliharibiwa, 21 kati ya hizo zikiwa katika Wilaya ya Mkuranga.

“Bei ya kopa imepanda kutoka shilingi 10,000 hadi 30,000 kwa kilo moja, na maeneo ya mipakani imefikia shilingi 100,000. Hali hii imeongeza uharibifu wa miundombinu ya umeme,” amesema Kiobya.

Kiobya ameeleza kuwa oparesheni hiyo imepunguza uharibifu wa transfoma na kushauri kuwepo kwa sheria inayozuia wafanyabiashara kununua miundombinu ya serikali.

“Sheria hiyo itasaidia kukomesha biashara haramu na kuhakikisha huduma zinaendelea kufikia wananchi bila vikwazo,” ameongeza.

Miundombinu iliyokamatwa ni pamoja na nyaya za transfoma, vipuli vya DAWASA, na vifaa vya TRC, TTCL, na TANESCO. Serikali imeahidi kuendelea kufuatilia na kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo vya uhalifu.