Ulega ampa maua Samia ujenzi barabara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:16 AM Jan 02 2025
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.

RAIS Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Mbagala hadi Kongowe itakayopunguza foleni upande wa Kusini mwa Dar es Salaam.

Barabara hiyo itafungua fursa za kiuchumi kwa mikoa ya Kusini na kuondoa kero ya muda mrefu katika eneo la Mbagala hadi Kongowe, ikiwa ni mpango wa kitaifa wa Rais Samia kuboresha miundombinu nchini.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, jana akitangaza kuanza kwa mchakato wa upanuzi foleni ukanda huo, katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwandege, mkoani Pwani jana, alisema kipande cha barabara kitakachopanuliwa kwa muda mrefu kimekuwa kero kwa wananchi kwa kusababisha foleni za muda mrefu.

“Naomba kuwaambieni leo kwamba Rais amekubali ombi letu la kufanya upanuzi wa barabara hiyo na ameruhusu taratibu za zabuni kuanza. Sasa kero hii inakwenda kumalizika haraka na shughuli zenu za kiuchumi na kijamii sasa zitapata kasi mpya, alisema Ulega.

Alikuwa akizungumza katika Mkutano mkuu wa mwaka wa Jimbo la Mkuranga ambalo ni mbunge. Mkutano huo hufanyika mwishoni mwa mwaka kutokana na utaratibu ambao amejiwekea tangu awe mbunge.

Alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi mwezi Desemba, mwaka jana, alisema ujenzi wa barabara hiyo kuanzia eneo la Kokoto – Mbagala Rangi Tatu kuelekea Kongowe ni sehemu ya ujenzi mkubwa wa barabara unaoendelea nchini kote chini ya utawala wa Rais Samia.

Alisema kwamba mafanikio katika ujenzi wa barabara, madaraja, miradi ya umeme na mambo mengine unatokana na mafanikio ya kiuchumi ambayo Tanzania imeyapata kwenye utawala wa Rais Samia.

“Waswahili wanasema usione vyaelea vimeundwa. Huwezi kujenga barabara namna hii, ukajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, ukajenga SGR bila kuwa na uchumi unaoruhusu hayo. Rais wetu ni wa kipekee na maono na miongozo yake ndiyo inafanya tutambe namna hii,” alisema.

Aidha, mwenendo wa kiuchumi unaoendelea sasa, kuna uwezekano wa kero nyingi za barabara kupungua sana wakati wa utawala wa Rais Samia na kusema anatarajia atapata kura nyingi kutoka kwa Watanzania kwenye uchaguzi wa mwaka 2025 kwa sababu rekodi yake inajieleza.

Katika mkutano huo ambao mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, baadhi ya viongozi waliohudhuria walikuwa ni madiwani, wenyeviti wa mitaa na viongozi wengine wa chama na serikali katika Wilaya ya Mkuranga na Mkoa wa Pwani kwa ujumla. 

Pamoja na mambo mengine, Ulega alieleza mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika wilaya hiyo ikiwamo ongezeko la shule za msingi, vituo vya afya na kuimarika kwa huduma za kijamii.

Mbele ya wananchi wa Mkuranga, Ulega alitangaza pia kuanza kwa ujenzi wa jengo la ghorofa litakalotumika kufundisha wanafunzi katika Shule ya Msingi Mwandege.

Alisema hatua hiyo imezingatia ukweli kwamba eneo la Mwandege lina idadi kubwa ya watu na kwa ukubwa wa eneo iliko sasa, namna pekee ya kukabiliana na ongezeko la wanafunzi ni kujenga shule za ghorofa zitakazotumia eneo dogo kusomesha wanafunzi wengi zaidi.