Tabora hasira sasa kwa Namungo FC

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:24 AM Feb 05 2025
Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala

BAADA ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Simba, Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, timu ya Tabora United, leo itashuka tena uwanjani hapo ikiwa na lengo la kumalizia hasira zake dhidi ya Namungo FC.

Wakati Tabora ikiuchukulia mchezo huo kuwa ni wa kutaka kuwafariji mashabiki wake kwa kipigo, Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, alisema wapinzani wao wasichukulie kuwa utakuwa mchezo rahisi kwao.

Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala, alisema hawatokubali tena matokeo mabaya kwenye uwanja wao wa nyumbani, na hasira zote za kufungwa na Simba watazimalizia kwa Namungo.

"Matokeo mabaya dhidi ya Simba yasituvunje moyo, na wala yasitutoe kwenye reli, tunajua mzunguko wa pili hatukuuanza vizuri, lakini tunawataka mashabiki wetu waje kwa wingi uwanjani, tunawahakikishia kuwa tunafanya kila njia ili tuwafute machozi," alisema Christina.

Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, amesema maandalizi yamekamilika na wachezaji wake wako tayari kwa mchezo huo ambao alisema utakuwa mgumu.

"Tunakwenda kucheza na Tabora United, tunawaheshimu, ni moja ya timu nzuri sana, imeimarika kwenye kila idara, ni washindani, tunacheza nao haijalishi wametoka kufungwa na nani, japo tunajua ni ngumu kwa sababu hawatotaka kufungwa tena.

"Sisi tunaingia tukiwa na kikosi chetu ambacho kimeimarika kwa kuongeza baadhi ya wachezaji kwenye dirisha dogo, nimewaona, nadhani wataongeza kitu," alisema Mgunda.

Wakati Tabora United, ikiwa kwenye nafasi ya tano na pointi zake 25, Namungo inakamata nafasi ya 12, ikiwa na pointi 17, zote zikiwa zimecheza michezo 16.

Mechi nyingine itapigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma, wakati wenyeji, Dodoma Jiji wakiikaribisha Pamba Jiji.

Dodoma Jiji itaingia uwanjani ikiwa nafasi ya tisa na pointi zake 19, huku Pamba Jiji ikiwa nafasi ya 14 na pointi 12 ilizovuna hadi sasa.