MAKALA MAALUM: Neema yaja shule jirani na makaburi

By Sanula Athanas , Nipashe
Published at 10:16 AM Feb 04 2025
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Shule ya Msingi Lipumba.

SIKU chache baada ya Nipashe kuchapisha ripoti kuhusu madhila yanayowakumba wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Lipumba kutokana na kujengwa jirani na makaburi, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma umechukua hatua za dharura kukabili hali hiyo.

Kwa siku tatu mfululizo kuanzia Desemba 16 hadi 18 mwaka jana, gazeti hili lilichapisha ripoti maalumu ikiangazia madhara ya shule hiyo kujengwa jirani na makaburi ya kijiji.

Mwenyekiti Msaidizi wa Kamati ya Shule hiyo, Remista Ndunguru, katika mazungumzo na mwandishi wa habari hii juzi, alisema kuwa Januari 17 mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura alizuru shuleni Lipumba kujionea kilichoripotiwa na Nipashe.

"Mkurugenzi alikuja shuleni akiwa na wasaidizi wake. Walipofika, walikagua mazingira ya shule kisha wakawa na mazungumzo na uongozi wa shule, kijiji, parokia na baadhi ya wazee wa kijiji hiki ambao aliagiza wafike kumweleza historia ya makaburi yaliyo jirani na shule," alisema.

Mwenyekiti Msaidizi Remista alisema kuwa baada ya mazungumzo hayo na wazee wa kijiji, Mkurugenzi Kashushura alitoa maagizo matano kwa uongozi wa kijiji cha Lipumba na Kamati ya Shule hiyo ambayo alielekeza utekelezaji wake uanze siku hiyo hiyo (Januari 17, 2025).

Mosi; Uzikaji katika eneo la makaburi karibu na mpaka wa shule usifanyike tena. Miili izikwe katika makaburi hayo, lakini mbali na mpaka wa shule hiyo.

Pili; wanakijiji wasikatishe shuleni wakati wa kwenda makaburini na wakati wa kutoka makaburini. 

Tatu; madarasa mawili ya Shule ya Msingi Lipumba yenye uchakavu mkubwa yasitumike tena kwa sababu yanaweka hatarini usalama wa wanafunzi na walimu.

Nne, ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya walimu uanze mara moja shuleni Lipumba na miundombinu hiyo ijengwe mbali na mpaka wa makaburi na shule.

Tano; mkutano wa dharura wa kijiji uitishwe ili kuwaomba wanakijiji washiriki katika ujenzi huo (madarasa na ofisi ya walimu). Halmashauri inachangia Sh. milioni 50.

"Muda mfupi baada ya mkurugenzi na timu yake kuondoka shuleni, sisi Kamati ya Shule tuliona kumewekwa Sh. milioni 50 katika akaunti ya shule," alisema Remista huku akipongeza Nipashe kwa kuripoti kilichokuwa kinajiri shuleni Lipumba.

Remista aliendelea kueleza kuwa siku mbili baadaye (Januari 19, 2025) kuliitishwa mkutano wa kijiji ambao wanakijiji walipewa taarifa kuhusu ziara ya uongozi wa halmashauri na hoja ya ushiriki wao katika ujenzi wa miundombinu mipya ya Shule ya Msingi Lipumba.

Alisema iliridhiwa katika mkutano huo kila mwanakijiji mwenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 50, ashiriki ujenzi huo kwa kununua matofali matano ya saruji, matofali 3,500 yanatarajiwa kununuliwa na wakazi 700 wa kijiji cha Lipumba wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 50. 

Mchanga uliopelekwa shuleni Lipumba jana..jpg 38.23 KB

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, kijiji hicho kina wakazi 2,198 (wanaume 1,071 na wanawake 1,127), lakini kwa tathmini ya mkutano wa dharura wa kijiji ulioitishwa Januari 19 mwaka huu, kama ilivyotolewa ufafanuzi na Remista, ni wakazi 700 pekee wanaopaswa kununua matofali hayo, vigezo vikuu vilivyozingatiwa ni umri na uwezo wa kufanya kazi.

"Nguvu ya wananchi inahitajika kufanikisha ujenzi huu maana Sh. milioni 50 zilizotolewa na halmashauri, kwa hesabu iliyofanyika katika mkutano wa kijiji, ilionekana zinatosha kununua vifaa vya viwandani tu. Mchanga, kokoto na mbao lazima nguvu za mwananchi zitumike.

"Tumekubaliana matofali yanunuliwe kwa mzalishaji mmoja ili yasipishane mkubwa na ubora. Utaratibu unaotumika sasa, wananchi wanaungana, wakishafika 20 wanapeleka fedha kwa mzalishaji, matofali yao yanaletwa shuleni. Kwa huyo mzalishaji tofali moja anauza Sh. 2,300 pamoja na usafiri kutoka mjini Mbinga hadi hapa shuleni. Mwisho wa kuleta matofali shuleni ni Februari 10, mwaka huu," Remista alisema.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lipumba, Mathias Mpangala, alithibitisha taarifa iliyotolewa kwa Nipashe na Mwenyekiti Msaidizi Remista na kuongeza kuwa mbali na kuwekwa Sh. milioni 50 katika akaunti ya shule, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pia imewapatia vifaa vya kumalizia mradi wa darasa lenye vyumba viwili na ofisi ya walimu linalojengwa na wanakijiji shuleni Lipumba.

"Juzi (Jumamosi) mkurugenzi alileta mifuko 70 ya saruji, mabati matano ya kumalizia kofia ya darasa linalojengwa kwa nguvu za wananchi. Pia ameleta mchanga laini tripu mbili za lori na tripu mbili zingine za mchanga mgumu kwa ajili ya kumalizia kupiga lipu lile darasa na ofisi.

"Wananchi wameupokea vizuri mradi huu wa ujenzi wa madarasa. Zilipotolewa zile Sh. milioni 50, hesabu ilionesha kujenga madarasa mawili na ofisi ya walimu, zile fedha zisingetosha. Zingeishia kwenye baadhi ya vifaa tu, ndiyo maana wameamua kuchangia ujenzi wa madarasa hayo kwa kununua matofali yote ya ujenzi," alisema.

Katika kusimamia ujenzi huo wa madarasa na ofisi ya walimu, Mpangala alisema wana kamati mbili: Kamati ya Shule inasimamia matumizi ya Sh. milioni 50 zilizotolewa na halmashauri na Kamati ya Kijiji iliyoundwa ikiwa na wawakilishi wawili kwa kila kitongoji; wanasimamia ununuzi wa matofali. Kila mwanakijiji atakayenunua matofali, atathibitishwa na kamati hiyo ya kijiji.   

"Tunatarajia kuanza ujenzi wa madarasa mapya muda wowote. Kinachosubiriwa sasa ni taarifa ya wahandisi kutoka halmashauri ambao hivi karibuni walikuja shuleni kupima eneo la shule ili kuchagua eneo sahihi la kujenga madarasa hayo. Lengo letu ni kuondoka kule karibu na makaburi na mkurugenzi amesisitiza tujenge mbali zaidi na makaburi," Mpangala alisema katika mazungumzo na mwandishi wa habari hii jana.

UFAULU DUNI

Kama ilivyokuwa kwa matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba mwaka jana, Shule ya Msingi Lipumba haijafanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa Upimaji Darasa la Nne Mwaka 2024.

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa Januari 4, 2025 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Said Mohamed, Shule ya Msingi Lipumba ilikuwa na watahiniwa 52. Kati yao, hakuna aliyefaulu kwa daraja "A" wala "B", 15 wamepata daraja "C", 33 daraja "D" na wamefeli, kwa maana wamepata daraja "E", hivyo wanapaswa kukariri darasa.

 

Mchanganuo wa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Upimaji Darasa la Nne Mwaka 2024 katika Shule ya Msingi Lipumba. CHANZO: NECTA, Januari 4, 2025.