LICHA ya mafanikio yanayopatikana kwenye Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Kamati ya Bunge ya Miundombinu imesema matatizo ya kiusanifu ya injini za Airbus A220-300 ambazo zimekuwa zinapata hitilafu mara kwa mara, yanasababisha kukosa mapato wastani wa Sh. bilioni 127.3 kwa mwaka.
Akiwasilisha bungeni jana taarifa ya mwaka ya kamati hiyo kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Moshi Kakoso, alishauri serikali iharakishe upatikanaji injini mbadala za ndege aina ya A220-300 na pia itafute namna bora ya kuhakikisha ndege hizo zinaleta faida kwa nchi.
Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine ni upatikanaji vipuri kutokana na kushuka kwa uzalishaji vipuri hivyo duniani kutokana na athari za UVIKO-19.
Alisema ATCL pia inakabiliwa na uhaba wa marubani, hususan marubani viongozi, na wahandisi wenye leseni ya kuruhusu ndege kuruka baada ya matengenezo kukamilika.
Vilevile, kiongozi huyo wa kamati alisema kuna madeni yanayotokana na mkataba wa ukodishaji ndege kati ya ATCL na TGFA. Deni ya nyuma la TGFA ni Sh. bilioni 429 hadi Juni, 2024 na deni la taasisi za serikali ni Sh. bilioni 64 huku madeni ya wazabuni yakiwa Sh. bilioni 18.
"Serikali ifute deni la TGFA la Sh. bilioni 429, isimamie taasisi nyingine za serikali kulipa Sh. bilioni 64 kwa ATCL na kulipa madeni ya wazabuni Sh. bilioni 18 ili kuondoa changamoto ya madeni ya nyuma yanayolikabili shirika," alisema.
Mwenyekiti huyo alishauri serikali iendelee na mchakato wa kuhamisha ndege kutoka TGFA kwenda ATCL na isimamie kuboreshwa sheria ya uanzishwaji ATCL ili itambulike kama kampuni badala ya shirika la umma.
UTAPELI MTANDAONI
Vilevile, alisema suala la utapeli na uhalifu mwingine wa kimtandao limeendelea kuwa tatizo nchini, jambo linalopaswa kupatiwa ufumbuzi wa kina.
"Serikali iimarishe udhibiti wa uhuru wa mitandao kwa kuzingatia umuhimu wa demokrasia yenye mipaka; ihakikishe TCRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, inaweka mikakati madhubuti inayozihusisha kampuni za simu kukabiliana na uhalifu wa kimtandao," alisema.
Aliongeza kuwa katika kudhibiti uhalifu wa mitandao ya mawasiliano, serikali inapaswa kuhakikisha kampuni za simu zinawajibika ipasavyo katika kutoa nafuu za kisheria kwa waathirika wa uhalifu wa kimtandao.
MADENI POSTA
Kakoso pia aliitaka serikali ibebe deni inalodaiwa na Shirika la Posta Tanzania la Sh. bilioni 54 ili kusafisha mizania ya shirika na kuliwezesha kukopesheka.
Alisema serikali inapaswa pia kuongeze kasi ya kutekeleza ujenzi wa minara ya mawasiliano, hasa maeneo yaliyoainishwa kuwa na mahitaji maalum, akitolea mfano barabara kuu, mbuga za wanyama, mipakani na mapori tengefu ili kukuza shughuli za utalii na kuboresha usalama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED