TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga, imeokoa kiasi cha fedha Sh. milioni 137.8 za mauzo ya viwanja katika Manispaa ya Kahama, kutokana na baadhi ya waliomilikishwa viwanja hivyo, kutolipa gharama halisi.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, hayo yamebainishwa, leo Februari 4, 2025 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, kwa kipindi cha robo ya pili kuanzia Oktoba hadi Desemba 2024.
Amesema kwa kipindi hicho wamefanikiwa kuokoa fedha hizo, ikiwa ni sehemu ya mauzo ya viwanja 29 vilivyopimwa na Manispaa ya Kahama mwaka 2019, na kwamba katika viwanja hivyo ilitolewa gharama halisi ambayo wananchi wangepaswa kulipa, huku viwanja vitatu vikilipwa fedha halisi na 26 malipo yakiwa siyo sahihi.
“Manispaa ya Kahama, ilikuwa ikimiliki ardhi katika maeneo ya kimkakati eneo la Phantom na mwaka 2019 iliamua kupima eneo hilo na kuuza viwanja kwa mtu yoyote anayehitaji, vilipatikana viwanja 29 ambavyo vilipaswa kumilikishwa kwa wananchi kwa gharama ya Sh. 15,000 kwa mita moja ya mraba na viwanja vya biashara Sh. 20,000,” amesema Kessy.
“Mwaka 2024 TAKUKURU kupitia vyanzo vyetu vya siri tulipata taarifa kwamba, baadhi ya wananchi wamemilikishwa viwanja hivyo bila ya kulipa gharama zilizohitajika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Manispaa ya Kahama.
“Tulibaini kuwa kati ya viwanja 29 ni viwanja vitatu pekee wamiliki wake walilipa malipo halali, lakini 26 havikulipwa kwa gharama halisi vyenye thamani ya Sh. milioni 800,” ameongeza.
Amesema baada ya kubaini hilo, waliweza kuwafikia wamiliki wa viwanja hivyo 26 na kuwataka walipe gharama halisi ya mauzo ya viwanja hivyo au vitangazwe upya.
Baada ya agizo, Kamanda Kessy, alisema watu hao walikubali kufanya malipo kama walivyopaswa na Sh. milioni 137.8 zimeshalipwa kati ya Sh. milioni 800, huku wakiendelea kufuatilia fedha zingine zilizobaki Sh. milioni 662.2, ili kuhakikisha viwanja vyote vinalipiwa na fedha zake na kuingizwa serikalini.
Aidha, kwa upande wa dawati la uchunguzi walipokea malalamiko 38 na yaliyohusu rushwa ni 20 kati ya hayo na kwamba uchunguzi unaendelea, na wamejipanga pia kuzuia vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi mkuu ambao utafanyika mwaka huu.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vyovyote vya vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na miradi ya maendeleo, ili hatua za haraka zichukuliwe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED