MIAKA 30 YA BEIJING; ‘Liwike lisiwike uwezeshaji watoto wa kike haukwepeki’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:06 PM Feb 04 2025
 Ndoa za watoto ni suala lisilokubalika na maazimio ya Beijing
Picha: Mtandao
Ndoa za watoto ni suala lisilokubalika na maazimio ya Beijing

KUKOSOA juhudi za kuwawezesha watoto wa kike kwa madai kuwa zinalenga kufanya mapinduzi ya kufanikisha wanawake kutawala wanaume kunaanza kusikika.

Ni maoni yanayosikika miongoni mwa wanaopinga harakati za kuwainua wasichana na kuondoa mifumo kandamizi inayosababisha wawe mbumbumbu, maskini na kuendelea kuumizwa na ukatili wa kijinsia.

Hisia hizo zinatumiwa na watu wanaobanwa na lawama za kushindwa kuondoa unyanyasaji na misemo hiyo inadhihirisha kuna baadhi ya Watanzania hawataki kuona maisha ya mwanamke yakiboreshwa.

Mazoea ndani ya miongo mingi ya unyanyasaji wanawake na watoto inasababisha kuwaza kuwa kuwezesha wasichana ni mkakati wa kuwaandaa kuwakandamiza wanaume, wakati sivyo.

Balozi Getrude Mongella, Mwenyekiti wa Mkutano wa Beijing uliofanyika 1995 nchini China ambao leo umetimiza miaka 30, anachambua  hoja hiyo.

Ajenda kuu ya mkutano huo ni kuona dunia isiyo na ubaguzi wa kijinsia, kadhalika uwezeshaji wanawake na mtoto wa kike kwa hali zote unafanikiwa, anafafanua.

Balozi Getrude anakiri kuwa Beijing imeleta mapinduzi makubwa ya kifikra kwa kuwezesha serikali kutambua kuwa wanawake na wanaume wana haki sawa kama raia wa dunia moja.

Aidha, kutambua kwamba, wanawake ni wakazi wa dunia hii kama wanaume na kwamba dhamira ya mkutano haikuwa kubadilisha mfumo kandamizi na kusimika utaratibu kandamizi mwingine ili wanawake wachukue nafasi ya kunyanyasa wanaume.

Anasema lengo la mkutano na utekelezaji wa maazimio ni kujenga usawa wa jinsia kwa wanawake na wanaume, watoto wa kike na wa kiume bila ubaguzi.

MTOTO WA KIKE KWANZA

Kumwezesha si kukurupuka ni moja ya masuala 12 yaliyobainishwa katika tamko la Beijing mwaka 1995, baada ya kubaini kuwa mifumo kandamizi inawaathiri watoto, lakini kwenye mfumo dume mtoto msichana anaatharika maradufu.

Mfano, anabaguliwa hana haki ya kurithi, kielimu mwanaume anapendelewa zaidi asome, anafanyiwa ukatili wa kimwili, hukeketwa, kubakwa, kuozwa utotoni na kunyimwa haki nyingi za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Mathalani, Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022, inaonyesha kuwa mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni, Songwe ikiwa kinara yenye asilimia 45.

Inamaanisha kila watoto wa kike 100, karibu nusu au 45 wamenyanyaswa na kupewa mimba utotoni.

Ruvuma ni ya pili kwa asilimia 37, Katavi 34, Mara 31 na Rukwa asilimia 30.
 Hizo si habari njema baada ya miaka 30 ya Beijing inayosisitiza usawa wa kijinsia, uwezeshaji mtoto wa kike na maendeleo endelevu kwa wote. Hivyo kuwezesha watoto wa kike si hiari ni lazima.

Profesa Ruth Meena kutoka Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi, anafafanua maana ya kuwezesha mtoto msichana kuwa ni kumjengea uwezo wa kuuthamini mwili wake, kuulinda utu wake, kuutetea na kukataa kutumiwa kuumizwa iwe kimwili, kisaikolojia au kiuchumi.

Anafafanua kuwa binti aliyejengewa uwezo anathamini utu wa wote wakiwamo watoto wa kiume, hawanyanyasi, kukandamiza wala kuwadharau wengine, bali ni mtetezi wa haki zake na za binadamu.

Anasema uwezeshaji hauathiri wala kupokonya uwezo wa watoto wa kiume kwa sababu wamelelewa na kukuzwa kwenye mazingira na fikra za kuheshimu ndugu wa kike kuanzia mama zao hadi shangazi.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika kituo cha elimu cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima cha Tumbi Sekondari, mkoani Pwani, wanaorudi darasani baada ya serikali kuwawezesha waendelee na masomo ni mashahidi.

Wanaamini kuwa kupata mimba si mwisho wa maisha kwa sababu wamepata nafasi ya pili na sasa wanatimiza ndoto zao bila kukatishwa tamaa, kwani mtoto wa kike ameona alipokosea, akipaepuka na sasa yuko tena shule.

“Baada ya kupata mimba nilirejea nyumbani nikawaomba msamaha wazazi, wamenilea na mwanangu nilipojifungua. Baada ya miaka miwili wamenitafutia shule ninaendelea na masomo.” Anasema, mwanafunzi wa taasisi hiyo ya elimu, kituo cha Tumbi Sekondari, jina tunalihifadhi.

Kuanza kwake masomo ni uwezeshaji wa watoto wa kike kupitia program ya‘re-entry’ inayolenga kuwarejesha shuleni wasichana wanaokatizwa masomo kwa sababu yoyote, mpango unaoanzishwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwanafunzi mwingine anaeleza kwamba baada ya kupata mimba alifukuzwa na baba yake akakimbilia kwa mjomba aliyemlea hadi kujifungua na sasa amemsajili kituo cha Tumbi Sekondari anasoma.

Mifumo kandamizi bado inajitokeza, licha ya serikali kuruhusu wasichana warudi shuleni baada ya changamoto kama mimba, kukosa ada au umbali wa shule inaendelea kuwazuia ni wakati wa kubadilika jamii iwaunge mkono watoto wa kike kuboresha maisha yao. Ikumbukwe wanasoma bila malipo serikali ikigharamia elimu yao.

Watetezi wa haki za mtoto wa kike wanasisitiza msichana akiwezeshwa haathiriki na mifumo au taratibu kandamizi mfano, kutoka mikoani kupelekwa mijini na kwenye majijini makubwa kuwa mfanyakazi wa ndani.

Akielimishwa na kuwezeshwa atapinga kubakwa na waajiri, watoto au ndugu zake wanaume, kupigwa, kunyimwa mshahara na kutumikishwa kama punda.

Anasema Farida Jackson, Ofisa Miradi wa asasi ya Initiative for Domestic Workers, inayotetea haki za watumishi wa ndani mkoani Pwani.

“Akielimishwa na kuwezeshwa atataka mazingira na kazi zenye staha na usalama, atadai mkataba wa ajira, atatoa taarifa akidhalilishwa na kutetea haki zake hata mahakamani.”

“Zama lazima zibadilike siyo tena wakati wa kuwaacha watoto wa kike kutumiwa kingono nyumbani kwa watu mijini, wengine kwenye madanguro au ndani ya vibandaumiza mitaani na ajenda ni moja ya elimu na kuwawezesha ili sauti za wasichana na wanawake zisikike kwenye majukwaa makubwa kwa madogo kushangilia usawa wa kijinsia.” Anasema Farida.

Wakiwezeshwa na kuelimishwa jamii haitaendelea kusikia habari za manusura wanawake na watoto wanaoishi na VVU na UKIMWI baada ya kupitia  ukandamizaji na unyanyasaji kingono na kijinsia.

Kadhalika, mambo yatabadilika si kuwaona wakiishi kwa msaada wa mashirika ya kijamii na kupewa huduma za ushauri wa kisaikolojia, mafunzo na ujuzi wa maisha, badala yake watajitambua na kuepukana na madhila hayo. Huku wakiishi maisha bora kama raia bora wa dunia hii na Tanzania kama inavyoainisha Dira ya Maendeleo ya 2050, kuwa ni maisha bora kwa kila Mtanzania.

LA MUHIMU

Kuwa na bajeti za kijinsia, mfano ujenzi wa visima vya maji na vyoo vya wasichana vilivyo na vyumba maalumu vya kujisitiri wanapohitaji huduma hiyo, kama wanavyohimiza wanaharakati.

Uwezeshaji wa wanawake na watoto wa kike utaleta kujitambua na kunufaika na fursa za maendeleo zilizopo.

“AZAKI na serikali zikiwawezesha kujitambua watajua kuwa kazi yao si kutumiwa kuburudisha wengine.

 Mfano kwenye sekta zinazokua kwa kasi za sanaa,burudani na utalii watabadilika kujua kuwa jukumu lao si kuuza vinywaji, au kuburudisha zaidi. Watatumia fursa kujiendeleza na kumiliki vitega uchumi.” Anasema Najaha Bakari, Msemaji wa Baraza la Michezo la Taifa.

Anasema watakuwa watunga nyimbo si kuimba za wenzao, waandishi wa sinema akikumbusha kuwa uwezo mdogo kiuchumi, mapato duni na kukosa elimu vinachochea ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.

Ni wakati wanaohofia juhudi za kuwezesha watoto wasichana washiriki kampeni za kuwashirikisha wazazi, walezi na jamii kubadilisha mtazamo huo na kuhimiza umuhimu wa elimu na maisha bora kwa watoto wote, bila ubaguzi wa kijinsia.

Elimu na uwezeshaji vinafanikisha kutambua na kuibua vipaji vya watoto wa kike, kuwajenga na kuwaendeleza kwenye eneo wanalolipenda na kulimudu ili walitumie kuendeleza maisha yao kwenye dunia ya sasa yeny furusa nyingi zinazotokana na vipaji.

JUHUDI KITAIFA

Tanzania imepiga hatua katika miaka 30 baada ya Azimio la Beijing kuwezesha watoto wa kike na kutokomeza ubaguzi wa jinsia, udhalilishaji na unyanyasaji watoto mfano, ipo sheria ya makosa ya kujamiiana ya 1998, inayoharamisha na kuadhibu ukatili kama ukeketaji na ubakaji.

Aidha, Zanzibar imeanzisha mahakama ya maalumu ya udhalilishaji Juni 2021 kusikiliza kesi za ukatili dhidi ya watoto.

Kuna sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inayobainisha na kulinda haki za mtoto. Kadhalika

Mahakama Kuu na ya Rufani zilibatilisha vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya 1971 inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa chini ya miaka 14.