NAHODHA wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala', amesema kwa sasa wameingia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ambapo hawatakiwi kufanya makosa yoyote yatakayowafanya kudodosha pointi.
Tshabalala amesema kutokana na umuhimu huo, kila mchezo kwao wanauchukulia kwa umuhimu mkubwa kuhakikisha wanavuna pointi tatu.
Akizungumza na Nipashe jana muda mfupi baada ya kutoka bungeni walipoalikwa kwenda kupongezwa kwa kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, alisema watahakikisha wanazidi kupambana na kuongeza umakini.
"Tumeingia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, ni wa lala salama, kila timu inapambana kuhakikisha inafanya vizuri ili kuangalia mwisho wa mzunguko huu itakuwa kwenye nafasi gani, Simba tunalifahamu hilo, na sisi tunazidi kuongeza umakini kuhakikisha tunafanya vizuri.
"Kila mechi kwetu kwa sasa ni muhimu na tunaicheza kwa umakini mkubwa, hii ni hatua ambayo ukipoteza pointi inakugharimu sana…, kama wachezaji tutaendelea kupambana na kuhakikisha tunapata ushindi kila mchezo," alisema Zimbwe.
Baada ya juzi Simba kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, kesho itashuka tena uwanjani kucheza na Fountain Gate mkoani Manyara.
Mpaka sasa Simba wanaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 43 wakifuatiwa na watani zao, Yanga wenye pointi 42 huku Azam FC wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 36.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED