Ramovic kusaka ushindi wake wa saba Ligi Kuu

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:24 AM Feb 05 2025
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic

AKIWA tayari ameiongoza timu yake kupata ushindi kwenye michezo sita mfululizo ya Ligi Kuu aliyoisimamia akiwa Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, leo ana kibarua kingine cha kusaka ushindi wa saba kwenye mchezo dhidi ya KenGold FC utakaopigwa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.

Yanga inawakaribisha KenGold huku ikitoka kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar juzi kwenye uwanja huo.

KenGold wanawakabili Yanga leo huku wakiwa na kikosi kilichoboreshwa kwa kuongezwa nguvu baada ya kufanya usajili mkubwa katika dirisha dogo la Januari, ambapo kina baadhi ya nyota wakubwa wakiwamo mchezaji wa zamani wa Yanga na Simba, Bernad Morrison na Kelvin Yondani.

Hata hivyo, taarifa za ndani zinadai Morrison anaweza akaukosa mchezo wa leo kutokana na kuwa majeruhi.

Kocha wa Yanga, Ramovic akizungumzia mchezo wa leo, jana alisema watajitahidi kutumia nafasi katika mipira itakayodondoka nyuma ya mstari wa mabeki wa wapinzani wao.

Alisema anaamini mchezo utakuwa mgumu kutokana na maboresho ya kikosi cha wapinzani wao hao, lakini lazima wapambane kupata ushindi.

"Yanga tumechukua ubingwa wa Ligi Kuu misimu mitatu mfululizo, tunataka ubingwa wa nne, sasa ili kufikia hapo ni lazima kushinda mchezo huu wa kesho (leo), tunatakiwa kupambana, kutumia vizuri nafasi tutakazozitengeneza, lakini pia kuwa na nidhamu kwenye kujilinda," alisema.

Aidha, Ramovic amegusia kuhusu mchezaji wake mpya, Jonathan Ikangalombo ambaye bado hajaanza kuichezea timu hiyo tangu kusajiliwa kwake kwenye dirisha dogo.

"Tumeona bado hajawa fiti kucheza, hatuwezi kulazimisha acheze kwa haraka, anaweza kupata majeraha, taratibu tunamweka fiti na atakapokuwa tayari ataitumikia timu," alisema.

Kwa upande wa Kocha wa KenGold, Omari Kapilima, alisema ana imani na kikosi chake kutokana na maboresho waliyoyafanya.

"Tumeongeza wachezaji wenye uzoefu mkubwa na Ligi Kuu, nina imani mchezo wa kesho tunaweza kupambania na kuzipata pointi tatu," alisema Kapilima.

Aliongezea kuwa hawataweza kumtumia Morrison kwa sababu ni majeruhi, anaendelea kupona.

KenGold inakutana na Yanga huku ikiwa inaburuza mkia kutokana na kujikusanyia pointi sita pekee katika michezo 16 waliyocheza, wakizidiwa ponti 36 na wapinzani wao hao waliopo kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo.