KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameonekana kukoshwa na idadi kubwa ya mashabiki wa soka wanaojitokeza mikoani, akisema imekuwa chachu ya wachezaji wake kucheza kwa kujituma na kupata ushindi kwa asilimia 100 kwenye michezo ya ugenini ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imekuwa kama ipo nyumbani.
Akizungumza jijini Dodoma jana, ambako timu hiyo imeweka kambi ya muda kabla ya kuivaa Fountain Gate, katika mechi ya raundi ya 17 ya Ligi Kuu itakayopigwa kesho, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, kocha huyo alisema ameshangazwa na idadi kubwa ya mashabiki wanavyojitokeza kwenye viwanja vya mikoani, na cha ajabu zaidi ni kwamba zaidi ya asilimia 90 wamekuwa wakiishangilia Simba kwa nguvu zote, kitu ambacho kinamfanya yeye na wachezaji wake kufanya kila juhudi kuhakikisha wanaondoka uwanjani na furaha baada ya mchezo.
"Nimeona kwenye michezo mingi mikoani, kumekuwa na mashabiki wengi uwanjani na wanakuwa wanatushangilia sisi, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mashabiki walitia fora, walijitokeza kwa wingi zaidi, uwanja ulijaa sana, na karibuni wote walikuwa upande wetu, utagundua hilo bao linapofungwa, uwanja mzima unasimama kushangilia, tulikuwa ugenini, lakini ni kama nyumbani tu, hili pamoja na mambo mengine ya ufundi na mifumo, lakini nalo kiasi kikubwa linatusukuma sana kupata ushindi," alisema.
Simba imeshinda mechi zote nane ilizocheza ugenini mpaka sasa, ikiwa kinara wa kushinda mechi nyingi za ugenini mpaka sasa.
Kwa mujibu wa Kitengo cha Takwimu za Michezo Nipashe (KTDMN), Simba imeshinda mechi za ugenini dhidi ya Azam FC mabao 2-0, bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Prisons, Mashujaa FC, Pamba Jiji na Singida Black Stars, 5-2 dhidi ya Kagera Sugar, na 3-0 dhidi ya Tabora United.
Fadlu aliwashukuru mashabiki wa soka mkoani Tabora, akiwataka na wa Manyara kufanya kama walivyofanya wenzao ili wawape zawadi ya ushindi.
"Nadhani hata Manyara itakuwa kama Tabora, ningeomba iwe zaidi, na sisi tutawapa zawadi ya ushindi kwani tumedhamiria kwenda kuchukua pointi tatu zingine," alisema Fadlu.
Wakati huo huo, Daktari wa Simba, Edwin Kagoba, amewatoa hofu wanachama na mashabiki wa klabu hiyo juu ya afya ya Kibu Denis, ambaye aliumia kwenye mchezo uliopita.
Alisema japo kuna wasiwasi kama atatumika au la kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Fountain Gate, lakini hajapata majeraha ya kumweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
"Ni kweli mchezaji wetu Kibu alipata matatizo kwenye mguu wake wa kushoto katika mchezo dhidi ya Tabora United. Alikuwa na shida sehemu mbili, kwenye 'enka', na sehemu ya robo tatu ya chini ya mguu, hali yake kwa sasa iko vizuri, anaendelea na matibabu, yuko kwenye hatua ya pili ya matibabu, tunategemea leo (jana) au kesho (leo), atakapopita kwenye hatua zote za matibabu anaweza kuwapo kwenye mchezo wetu ujao.
"Ila hii ni nusu kwa nusu kuwapo, kuna vitu tunaviangalia leo na kesho, lakini niwatoe hofu wanachama na mashabiki wa Simba kwamba hali yake si mbaya si ya kumweka nje muda mrefu," alisema daktari huyo.
Wachezaji, benchi la ufundi na pamoja na Uongozi wa klabu hiyo, jana walilitembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano linaloendelea na vikao vyake jijini Dodoma.
Simba iliweka kambi ya muda jijini humo, ikitokea Tabora kujiandaa na mchezo wa kesho dhidi ya Fountain Gate, mkoani Manyara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED