DONALD Trump, ndiye Rais wa Marekani wa 47 ambaye tangu aingie ofisini wiki mbili sasa amekuwa gumzo duniani, akigusa nchi zinazoendelea na zilizoendelea.
Mashirika, watu binafsi, taasisi za umma na serikali za nchi zinazoendelea na zilizoendelea zimepata ‘meseji’ ya msimamo wa Marekani kutoka Ikulu ya White House, ambayo aliirejea tena Januari 20, mwaka huu.
Baada ya kuapishwa tu, alitia saini msururu wa hatua za kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kutangaza hali ya dharura ya kitaifa katika mpaka wa Marekani na Mexico na kuzitaja kampuni za dawa za kulevya kama mashirika ya kigaidi.
Kadhalika, amewageukia wahamiaji wasio na vibali wanaoishi Marekani. Kupitia Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE) pamoja na Operesheni ya Utekelezaji na Uondoaji, anasema kuanzia Novemba mwaka jana, watu 1,445,549 kati yao Watanzania 301 ambao si raia wataondoshwa nchini humo.
Miongoni mwa raia wanaoondolewa ni kutoka nchi 108, wakiwamo 8,946 kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambao wengi ni Wasomali wanaodaiwa kufikia 4,090.
Trump anatimiza alichokiahidi kwamba atawahamisha maelfu ya wahamiaji wasio na vibali, kuondoa urasimu wa serikali, kupunguza kodi, na kuanzisha ushuru mpya kwa bidhaa za kigeni.
Kadhalika, kusitisha misaada kwenye eneo la afya na alipoingia tu ofisini alianza na kutangaza kuondoa msaada wa Wamarekani katika Shirika la Afya Duniani (WHO), ambayo ilikuwa kauli yake ya kwanza siku chache tu baada ya kutawazwa rasmi.
"Hili ni jambo kubwa," anajivuna rais huyo kutoka Chama cha Republican, muda mfupi baada ya kutia saini amri ya kuanza mchakato wa kuiondoa Marekani kuwa mwanachama wa WHO.
Marekani ilichangia dola za Marekani bilioni 1.284 katika kipindi cha 2022-2023, kuwezesha WHO. Itakumbukwa Marekani na nchi nyingine na washirika hutoa fedha ili kukabiliana na dharura, kuzuia vitisho vya magonjwa kuenea katika mipaka na kuendeleza vipaumbele vingine muhimu vya afya duniani.
AFRIKA KUSINI
Rais Trump ametangaza hivi karibuni pia kusitisha ufadhili kwa Afrika Kusini.
Anasema hayo Jumapili iliyopita, kwamba Afrika Kusini, ilikuwa ikinyakua ardhi na kuwanyanyasa wakulima Wazungu, huku akitangaza kupunguza ufadhili wa siku zijazo kwa nchi hiyo hadi uchunguzi ufanyike.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, mwezi uliopita alitia saini muswada kwamba katika mazingira fulani, serikali haitatoa fidia kwa mali ambayo itaamua kuinyakua kwa maslahi ya umma.
AIGUSA BRICS
Trump, ameionya jumuiya ya nchi zinazoinukia kiuchumi ya BRICS, kwamba zikiacha matumizi ya Dola ya Marekani, ataziwekea ushuru wa asilimia 100.
Nchi za BRICS zinajumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini (South African) zilizojiunga pamoja kutetea maslahi yake dhidi ya mifumo mingine ya kibiashara.
Anasema matumizi ya dola ya Marekani hayaepukiki na iwapo nchi hizo zitajiondoa katika matumizi hayo kama njia ya malipo yake kimataifa, atiziongezea ushuru.
Anasisitiza kuwa Marekani haiwezi kukaa kimya na kuangalia namna BRICS inavyofikiria kuachana na matumizi ya dola kama sehemu ya malipo yake kimataifa.
Rais huyo wa Marekani ameongeza kuwa iwapo nchi hizo zitachukua hatua hazitauza wala kununua bidhaa kutoka Marekani.
Jumuiya hiyo ya BRICS inazijumuiya Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, mapema mwaka jana ilizikaribisha Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kujiunga huku Indonesia ikijiunga nao mwanzoni mwa mwaka huu.
BRICS iliundwa ili kukabiliana na dola, na kama mbadala wa kundi la mataifa saba yaliyoendelea kiuchumi duniani ya G7.
Rais wa Russia, Vladimir Putin amekuwa mara kwa mara akikosoa utegemezi wa dola ya Marekani na kutangaza nia yake ya kuanzisha mfumo huru wa malipo ndani ya Jumuiya ya BRICS.
China imeapa kulinda maslahi yake ya kitaifa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kwamba ushuru wa forodha wa asilimia 10 kwa bidhaa za China unaweza kuanza kutekelezwa kuanzia Februari mosi mwaka huu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning, anafafanua msimamo huo akisema taifa hilo, linaamini hakuna mshindi katika vita vya kibiashara au ushuru, hivyo litaendelea kulinda maslahi yake.
Aidha, Trump anaeleza kuwa kuna haja ya kurekebisha uwiano wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani, akidai umoja huo haununui bidhaa za kutosha za Marekani na hivyo angetafuta suluhisho kwa kuongeza ushuru au kuishawishi Ulaya kununua zaidi mafuta na gesi kutoka Marekani.
Wakati Rais wa Marekani anakuwa mkali kwa Afrika Kusini kwa upande mwingine sera yake kwa Afrika kwa ujumla haiko wazi.
Trump anasubiriwa kuzungumzia hatima ya Mkataba wa Ukuaji na Fursa kwa Afrika (AGOA) ambao unafikia ukingoni mwaka huu. AGOA inawezesha bidhaa za Afrika kuingizwa Marekani bila ushuru.
Kwa upande wake anataka anayenufaika ‘kutojihusisha na shughuli zinazodhoofisha usalama wa Marekani au maslahi ya sera za kigeni.”’
DW/BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED