JUMUIYA ya Wafanyabiashara Kariakoo imewasimika Mabalozi wa nyumba kwa nyumba kwa ajili kusimamia urasimishaji wa biashara, ili kuhakikisha kila mmoja anasajiliwa na kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN).
Lengo ni kuleta usawa katika kulipa Kodi.
Akizungumza wakati wa kuwasimika mabalozi hao leo Februari 04, 2025, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amesema mabalozi hao watasaidia kuhakikisha kunakuwepo na usawa katika kulipa Kodi kwa hiari kwa kuwezesha watu wote wanaofanya biashara Kariakoo kusajiliwa na kulipa Kodi inayostahili hali ambayo itaweka ushindani uliosawa sokoni.
Kamishna Mwenda amesema jukumu kubwa la TRA ni kusimamia ustawi wa biashara, ili ziendelee kukua na kuhakikisha kuwa hakuna biashara inayokufa na kwa Kariakoo ni eneo muhimu la biashara linalogusa mikoa yote na nchi jirani.
Amesema Kariakoo ni ukanda maalumu wa kikodi kutokana na kuwepo kwa walipakodi wadogo, wa kati na wakubwa hivyo ipo haja ya TRA kuwa karibu nao na kuwasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili.
Mwenda amesema changamoto za kisera zinazowakabili walipakodi tayari zimeundiwa Tume na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na zinafanyiwa kazi huku zile zinazotakiwa kushughulikiwa na TRA ambazo ni za kimfumo nazo zikiwa zinatatuliwa na mamlaka hiyo.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema milango yake ipo wazi muda wowote kwaajili ya walipakodi na yupo tayari kuwasikiliza kwa lengo la kuboresha mazingira yao biashara.
"Rais Dk . Samia Suluhu Hassan aliponiapisha alinipa majukumu na hayo ndiyo nayasimamia ikiwemo kusimamia na kukuza uendelezaji wa biashara na ustawi wake pamoja na kukusanya kodi kwa hiari pasipo kutumia nguvu, na jambo la heri mmekuwa tayari wakati wote kulipa kodi na hata wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga nao leo wamenithibitishia kuwa wapo tayari kulipa Kodi," amesema Mwenda.
Amewataka kuwafichua wote wanaokwepa kodi pamoja na wageni wanaofanya biashara zinazotakiwa kufanywa na wazawa maana vitendo hivyo vimekuwa vikidhoofisha ushindani ndani ya soko.
Kuhusu wamachinga kwenda Jangwani, Mwenda amesema watahakikisha wanaweka mazingira rafiki.
Mwenda amesema hakuna changamoto yoyote ya walipakodi nchini itakayokosa majibu huku akigusia suala la mizigo ya wafanyabiashara wa Kariakoo iliyokwama bandarini na kumuagiza Naibu Kamishna wa Forodha kushughulikia changamoto hiyo haraka.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema wanaandaa kanzi data ya wafanyabiashara wote wa Kariakoo na kuweka utaratibu wa pamoja na TRA katika kuwasajili, ili kuwapunguzia safari ya kuwafuata ofisini wakati wakijiandaa kuanza kufanya biashara saa 24.
Mpogolo amesema hatua ya Kamishna Mkuu wa TRA kwenda Kariakoo kirafiki ni jambo ambalo linaonyesha uhusiano na ushirikiano wa karibu baina ya mamlaka hiyi na wafanyabiashara.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severin Mushi, amesema wameamua kuweka mabalozi katika kila nyumba ili wasaidie kusajili wafanyabiashara na kuwezesha kila mwenye biashara Kariakoo kuwa na TIN namba, kuweka usawa katika ulipaji wa kodi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED