Zaidi abiria 900 wakwama mawasiliano reli kukatika

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 11:05 AM Jan 03 2025
Treni inayfanya safari kwenda  mikoa ya Kigoma Mpanda na Tabora.
Picha: Maktaba
Treni inayfanya safari kwenda mikoa ya Kigoma Mpanda na Tabora.

ABIRIA 901 na watumishi 30 wanaosafiri na treni kutoka mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora kwenda Dar es Salaam, juzi walikwama kwa zaidi ya saa sita kwenye kituo kikuu cha reli Dodoma baada ya mawasiliano ya Reli ya Kati kukatika.

Eneo lililokatika mawasiliano ni Godegoge wilayani Mpwapwa na Kidete, wilayani Kilosa, baada ya kujaa maji kutokana na mvua inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini. 

Adha hiyo imewakumba abiria waliokuwa wanatoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa Magharibi na kuulazimu uongozi wa Shirika la Reli nchini TRC, kukodi mabasi ili kusaidia wasafiri hao kuendelea na safari.

Mbwana Omary, mmoja wa abiria hao akizungumza na waandishi wa habari katika Stesheni Kuu ya Dodoma, alisema wametoka mkoani Kigoma juzi na kuwasili Dodoma jana usiku majira ya saa 7:00 usiku.

“Tumeanza safari kutoka Kigoma Desemba 31, lakini njiani tumekuwa na vituo vingi sana kila eneo tunasimama sana, lakini hapa Dodoma tulifika majira ya saa 7:00 usiku na kukaa kwa muda mrefu tulipouliza tukaambiwa tusubiri tutaambiwa nini kinaendelea.

“Tunashangaa asubuhi tunaambiwa kuwa tunaletewa mabasi kwa ajili ya kutuchukua kutuvusha eneo lenye changamoto hiyo na sisi wengine tulitaraji kuwahi mabasi yetu ya mapema, lakini hadi sasa tumeshakosa usafiri, kama mimi na wenzangu tunakwenda Tanga muda huu hatuwezi kupata usafiri tena,” alisema.

Aidha, alisema kukwama kwa treni kumeawathiri kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa baadhi ya gharama na kuiomba serikali kulifanyia kazi eneo hilo ambalo limekuwa kero kila mwaka.

“Hapa tulipo tayari tumetumia gharama kubwa na tangu tumekwama hapa usiku ule wa saa 7:00 hakuna huduma za msingi ambazo tumezipata,” alisema.

Zuwena Juma alisema wanawake pamoja na watoto wamepata usumbufu mkubwa kutokana na kukwama kawa treni hiyo kutokana na kukosa huduma za masingi.

Aliishauri serikali kutafuta mwarobaini ambao utasaidia kukabili hali hiyo ambayo imekuwa kero kwa abiria kila mwaka.

“Hili tatizo sio kama serikali hailifahamu kwani kila mwaka la mvua zitakapoanza kunyesha linatokea, hivyo serikali itafute namna ya kulikomesha hata kama kujenga daraja ili kuwaondolewa usumbufu Watanzania wanaotumia usafiri huu,” alisema.

Mkuu wa Stesheni ya Dodoma, Festo Mgomapayo alisema walisitisha safari ya treni hiyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa maofisa wao kuwa njia imejaa maji katika eneo hilo kutokana na mvua.

“Treni hii ilingia mkoani Dodoma kutoka Kigoma jana (juzi) usiku wa saa 8:00 na ilipofika hapa tayari tulishapata taarifa za njia yetu kujaa maji kutokana na mafuriko hivyo tusingweza ruhusu iendelee na safari wakati maji yamejaa kwenye njia hadi maji yapungue ili njia ionekane.

“Lakini leo (jana) asubuhi makao makuu wakaamua kuwa hawa abiria wasiendelee kubaki tu hapa hivyo yakakodiwa mabasi ambayo yatawabeba kwa ajili ya kuendelea na safari katika mikoa wanakokwenda.

“Pia, kuna treni yetu nyingine ambayo imezuiliwa kule Kilosa kwahiyo hawa wataenda kuitumia ile ya Kilosa kwenda Dar es Saalam na wale wengine wataletwa na mabasi haya hapa Dodoma kuendelea na safari katika mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa,” alisema Mgomapayo.

Wakati huo huo, kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa watatu kwa kosa la kuingilia miundombinu ya SGR kwa kutoa vitu muhimu, kuharibu na kuiba nyaya za shaba zenye urefu wa mita 10 zikiwa na thamani ya Dola za Kimarekani 38,581 (Sh. milioni 89.8) imeahirishwa hadi Januari 14, 2025.

Kesi hiyo iliahirishwa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Dodoma, Eligy Magalla, kutokana na hakimu ambaye alikuwa akisikiliza shauri hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Denis Mpelembwa kuwa na udhuru.

Washtakiwa hao ni Said Kapambwe mnyamwezi (38) mfanyabiashara mkazi wa Bahi, mshtakiwa wa pili ni Michael Ngayo Legayseki maarufu ‘Yakobo Mmasai’ (27) mlinzi mkazi wa Bahi Sokoni na mshtakiwa wa tatu ni Petro Merungwa Rengaisi (22), mlinzi mkazi wa Bahi.

Akiwasomea hati ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao Wakili wa Serikali Zubeda Lyaumi, alisema inadaiwa kuwa Oktoba 7, 2024 maeneo ya Bahi Sokoni, Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma watuhumiwa hao waliingilia miundombinu ya reli ya kisasa (SGR) kwa kutoa vitu muhimu, kuharibu na kuiba nyaya za shaba zenye urefu wa mita 10.

Awali, Wakili wa Serikali Josephat Mwinra, alidai upelelezi bado haujakamilika na kuiomba mahakama kuipangia tarehe nyingine.

Mshtakiwa namba moja Kapambwa anatetewa na Wakaili Meshack Ngamando aliiomba mahakama hiyo kuharakisha uchunguzi kwakuwa shauri hilo halina dhamana.