Lema aibuka na hoja nyingine, CHADEMA yasema haitekelezeki

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:35 AM Dec 31 2024
 Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.
Picha:Mtandao
Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimejibu hoja iliyotolewa na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema kuhusu uteuzi wa mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kupitia akaunti yake ya X, Lema alipendekeza jana kuwa Mkutano Mkuu wa chama hicho utakaofanyika mwezi unaonza kesho, utoke na jina la mgombea urais.

Lema pia alipendekeza mkutano utoe mamlaka kwa Kamati Kuu au Baraza Kuu la chama hicho kutafuta mgombea mwenza na kumthibitisha kwa niaba ya mkutano mkuu ili chama kitoke na jina la mgombea sambamba na viongozi wakuu wa chama hicho.

"Ingewezekana Mkutano Mkuu wa chama chetu utakaofanyika Januari, utoke na jina la mgombea urais na pia utoe mamlaka kwa Kamati Kuu/Baraza Kuu kutafuta mgombea mwenza na kumthibitisha kwa niaba ya Mkutano Mkuu ili chama kitoke na jina la mgombea sambamba na viongozi wakuu wa chama.

"Jambo hili ni muhimu kwa ajili ya 'branding' (kumtangaza kwa lengo kuongeza umaarufu) ya mgombea urais na masuala ya uratibu wa masuala ya kampeni na rasilimali fedha kwa mgombea.

"Pengine wazo hili likifanyiwa kazi, bila shaka tunaweza kumaliza salama zaidi na kupunguza kelele nyingi zisizokuwa na maana. Kamati Kuu inaweza kufikiri hivi," aliandika Lema.

Nipashe iliwasiliana na uongozi wa CHADEMA kuzungumzia hoja hiyo ya Lema, ukiwa na majibu kwamba hoja hiyo haitekelezeki kwa kuwa muda uliobaki kufikia Mkutano Mkuu wa chama ni mfupi.

"Ni maoni na ushauri wake kama mwanachama, yatapimwa kwa kuzingatia uzito wa hoja husika kwa wakati mwafaka," alisema John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA.

Mrema alimweleza zaidi mwandishi wa Nipashe, akisema: "Kuhusu utaratibu wa kumteua mgombea urais, Katiba yetu imeweka utaratibu. Ibara ya 7.7.16, kazi za Kamati Kuu ni kufanya utafiti wa wagombea urais na mgombea mwenza na kuwasilisha ripoti zake kwa Baraza Kuu la chama.

"Hivyo, kwa mujibu wa ibara tajwa hapo juu, ni wazi kuwa wazo lake halitekelezeki kwa huu muda mfupi ambao tumebakiwa nao kabla ya Mkutano Mkuu wa chama kufanyika."