MEYA wa Manispaa ya Mpanda mkoani hapa, Haidary Sumry ameomba serikali kutoa msamaha wa matibabu kwa watoto wanaolelewa katika vituo vya yatima ili waondokane na changamoto za kukosa huduma za matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Alisema hayo katika hafla ya kula chakula cha mchana na watoto yatima wanaolelewa katika cha malezi cha Kanisa Katoliki kilichoko kata ya Nsemulwa, Manispaa ya Mpanda, huku akikabidhi misaada ya kiutu na bima za afya za matibabu kwa watoto 20.
Alisema matunzo ya watoto ikiwamo kuwasaidia kupata huduma sahihi na bora za afya ni jukumu la wananchi wote, ikiwamo serikali, hivyo ipo haja serikali kuona namna ya kusaidia vituo hivyo kwa kutoa msamaha wa matibabu kwa kundi hilo.
Meya huyo aliongeza kuwa kinachopaswa kufanyika sasa ni ama kuwatengenezea bima maalumu zitakazowawezesha kupata matibabu mazuri na yenye uhakika au kutoa msamaha wa matibabu kwa kundi hilo.
Alisema zipo taarifa kwamba mazingira ya uendeshaji vituo hivyo ni magumu, baadhi ya watoto wamekuwa wanakumbana na vikwazo katika kupata huduma za matibabu.
"Hivi vituo vinasaidia tu kufanya kazi hii. Lilipaswa kuwa jukumu la serikali, hivyo kwa upendo na huruma tumwombe Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan aone uwezekano wa kusaidia vituo hivi kwa kutoa msamaha wa matibabu au bima maalumu zitolewe kwao," alisema.
Meya huyo pia alitoa wito kwa jamii, hususani wanawake ambao kila mwisho wa mwaka wanavunja vikoba na makundi mbalimbali, kutoa sehemu ya kile wanachopata kwa kusaidia makundi maalumu yenye uhitaji.
Awali, Mlezi kiongozi katika kituo hicho, Sista Rose Sungura alisema jamii inapaswa kuelewa kwa ni wajibu wa watu wote kuwalea watoto wenye uhitaji, wakiwamo yatima.
Hivyo, alitoa wito kwa wananchi wa Mpanda kujitokeza na kutoa misaada ya kiutu itakayosaidia kupunguza changamoto katika malezi ya watoto hao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED