Radi yaua watano wa familia moja

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 10:16 AM Dec 30 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga.

WATU watano wa familia moja katika kitongoji cha Nkangi, wilayani Chunya, mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi kwenye kambi ya kuchunga ng'ombe wakiwa wamelala, huku wengine watano wakijeruhiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo, akisema tukio hilo lilitokea saa 8:30 usiku wa kuamkia jana.

Kamanda Kuzaga alisema tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Nkangi, watu hao watano wa familia moja ya mfugaji Masiganya Scania (39) wakifariki dunia.

Aliwataja waliofariki dunia katika tukio hilo ni Balaa Scania (28), Kulwa Luweja (17), Masele Masaganya (16), Hema Tati (10) na Manangu Ngwisu (18), wote wakazi wa kijiji cha Nkangi. 

"Katika tukio hilo, watu wengine watano walijeruhiwa ambao ni Gulu Scania (30), Manyenge Masaganya (13), Seni Solo (13), Paskali Kalezi (16) na Huzuni Kalezi (19)," alisema Kamanda Kuzaga.

Alisema chanzo cha tukio hilo ni mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jana iliyoambatana na radi na kusababisha vifo vya watu hao na kujeruhi kadhaa.

Kamanda Kuzaga alisema majeruhi walikimbizwa katika Kituo cha Afya Isangawana kwa ajili ya matibabu na baadaye waliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali zao kuimarika.

Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Anna Mwakilima (24), mkazi wa Mbuyuni, wilaya ya Mbarali kwa tuhuma za wizi wa mtoto mwenye umri wa miezi miwili na nusu (jina la mtoto tunalihifadhi kwa sababu za kisheria).

Kamanda Kuzaga alisema kuwa Desemba 22 mwaka huu, Aneth Mgaya (20), mkazi wa kijiji cha Mwakaganga, wilayani Mbarali, aliibiwa mtoto wake mwenye umri wa miezi miwili na nusu na mwanamke ambaye alimfahamu kwa sura.

Alisema siku moja kabla ya tukio, majira ya saa 10 jioni, mtuhumiwa alifika nyumbani kwa Aneth na kuomba hifadhi ya kulala kwa madai kuwa alitokea mjini Mbeya na alikuwa anaishi kwa muda Ubaruku, Mbarali kwa ajili ya biashara ya vitenge.

Alieleza kuwa siku iliyofuata Desemba 22, 2024, saa moja asubuhi, Aneth aliamka na kutoka nyumbani kwake kwenda kununua vitafunwa eneo la jirani, huku akimwacha mtuhumiwa na watoto wawili. Baada ya kurejea nyumbani, hakumkuta mtuhumiwa wala watoto wake.

Kamanda Kuzaga alisema Aneth alitoa taarifa katika kituo cha polisi na ufuatiliaji ulifanyika na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.

Alisema kuwa juzi saa 12 jioni, katika kijiji cha Mbuyuni, kata ya Mapogoro, wilayani Mbarali, polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Anna Mwakilima akiwa na mtoto huyo ambaye hajamdhuru.