Watiwa mbaroni kwa tuhuma za mauaji

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 12:15 PM Dec 30 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda.

JESHI la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watuhumiwa wawili wanaodaiwa kumuua Editha Andeson (32), mkazi wa Kilimahewa, Manispaa ya Bukoba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda jana aliwataja watuhumiwa hao ni Mtalemwa Answali na Kenedi Mganyizi, wote wakazi wa Kashenye, kata ya Kashai, Manispaa ya Bukoba.

Kamanda Chatanda alisema watuhumiwa wote waliokamatwa, wanadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke huyo.

"Watu hawa walifanya kitu ambacho kimsingi ni cha kijinga, Edither alikuwa na mume ambaye ni bodaboda. Isivyo bahati, akawa na uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine ambaye walikuwa wanafanya kazi sehemu moja.

"Kwahiyo yule waliyekuwa wanafanya naye kazi sehemu moja, akaingiwa na wivu baada ya kuona ameanzisha tena uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine, yaani hawa wote wawili ni wezi, lakini kwa sababu ameanzisha mapenzi na mwizi mwingine, roho ikauma," alisema Kamanda Chatanda.

Alidai watuhumiwa hao walimuua mwanamke huyo kwa kutumia kamba ya mtandio.

Kamanda Chatanda alisema: "Baada ya kuingiwa na wivu, siku ya tukio, akamwita huyo mwanamke sehemu ambayo kwake aliona itakuwa rahisi kufanya tukio. Mara nyingi walikuwa wakikutana. 

"Akamkaba kwa kutumia mtandio halafu wakashirikiana na mwenzake kumtoa katika eneo hilo na kwenda kumweka katika eneo lingine ili asitambulike kirahisi.

"Chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi. Wakiwa katika uhusiano huo, Answari Mutalemwa alibaini kuwa mpenzi wake huyo ana uhusiano na mtu mwingine," alisema Kamanda Chatanda.

Alisema kitendo hicho kilimchukiza na kwa kushirikiana na wenzake waliamua kumuua Editha Anderson na kuchukua simu yake ya mkononi ili isipatikane.