Simba, Yanga mna deni kwa Rais Samia Suluhu

Nipashe
Published at 07:00 AM Aug 24 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha:Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

WIKI hii inayomalizika kesho imekuwa ya aina yake kwenye medani ya michezo hapa nchini, hususani soka.

Kumekuwa na shughuli nyingi za michezo ambapo Ligi Kuu Tanzania bara imeendelea lakini kitu kingine ni uwepo wa tamasha la kila mwaka la Kizimkazi linalofanyika visiwani Zanzibar.

Katika tamasha hilo wakati wa uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha michezo cha Suluhu Akademi, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa taarifa njema kwa klabu zetu kubwa, Simba na Yanga.

Rais Samia alidokeza kuwa lipo jambo linaloendelea kwa ajili ya klabu hizo ambazo mara kwa mara wamekuwa wakiiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la soka Afrika, CAF.

Rais Samia akizungumza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi wa kituo hicho, alisema amefanya mazungumzo na wadau na wawekezaji wakubwa hapa nchini kwa ajili ya kuzisaidia klabu hizo kongwe.

"Najua wadhamini au washika vilabu hivi wanafanya jitihada kubwa sana, lakini pamoja nao nimeongea na wadau, wawekezaji wetu wakubwa hapa, mmoja nimempa Yanga, mmoja nimempa Simba awasaidie," alisema Rais Samia.

Hili ni jambo zuri na la kupongezwa kwa Rais wa nchi kuona umuhimu wa kuziongezea nguvu klabu hizi ili ziweze kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.

Ingawa bado mambo hayajakamilika na wadhamini hawajatangazwa, lakini pindi itakapokamilika, klabu hizi zijue zina deni la kulipa kwa Rais Samia katika kuonesha shukrani kwa kuongezewa wadhamini.

 Nizikumbushe klabu zetu hizi, shukrani pekee na yenye kumbukumbu nzuri ni kuhakikisha mara baada ya mchakato mzima kumalizika, basi zijipange kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya kimataifa.

Rais ameona juhudi za klabu hizi katika kutafuta wadhamini iliwachangie kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa, ameona kuna haja ya kuzisaidia kupata wadhamini wengi zaidi ili safari yao ya kufanya vizuri kimataifa iwe nyepesi.

Tunampongeza Rais Samia kwa jambo hili, lakini tunazikumbusha klabu hizi kuhakikisha zinajipanga vizuri mara baada ya kupata wadhamini hao wafanye vizuri zaidi kimataifa.

Ni wazi kwa sasa klabu zetu hizi kucheza hatua ya robo fainali mashindano ya kimataifa, iwe Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho ni jambo la kawaida, zijiandae kumpa shukrani Rais kwa kuvuka hatua hiyo.

Lakini jambo lingine la kumpongeza Rais Samia ni ujenzi wa kituo cha michezo cha Suluhu Akademi kule Kizimkazi, ni wazi kituo hicho kikikamilika kitawapa nafasi na fursa vijana kukuza na kuendeleza vipaji vyao.

Ujenzi wa kituo hicho umejumlisha ujenzi wa viwanja mbalimbali vya michezo, ni jambo kubwa katika maendeleo ya michezo hapa nchini.

Tanzania ili kufikia ndoto ya kufanya vizuri siku moja katika mashindano mbalimbali, ni lazima tuwe na vituo kama Suluhu Akademi vingi zaidi ili kutoa fursa vijana wadogo kuanza kukuza na kuendeleza vipaji vyao.

Wito wetu, Watanzania watumie vizuri kituo hicho kuendeleza vipaji ili Tanzania izalishe vijana wengi mahiri kwenye michezo mbalimbali.