Kodi lazima ilipwe kuleta maendeleo

Nipashe
Published at 09:52 AM Aug 22 2024
Kodi
Picha: Mtandao
Kodi

MAENDELEO ya nchi hayawezi kupatikana bila kodi zinazokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.

Ujenzi wa barabara za kisasa, hospitali, shule na huduma nyingine muhimu anazotakiwa kuzipata mwananchi zinatokana na kodi ambazo serikali inakusanya.

Hata hivyo, matokeo ya kodi hizo ni lazima yaonekane ili wananchi waendelee kuona umuhimu wa kulipa kama inavyoonekana katika nchi nyingine zilizoendelea duniani.

Katika nchi zilizoendelea kodi hizo pia husaidia kuwatunza wazee ambao hawawezi tena kujitegemea na badala yake kulelewa kwenye nyumba za kutunza wazee.

Hata kwa wale wanaoweza kujitegemea, serikali zao huwalipa kiwango fulani cha pesa kila mwezi ili waweze kununua mahitaji muhimu na kulipa bili mbalimbali za huduma.

Mara nyingi malalamiko hujitokeza wananchi wanapoona wanakatwa kodi, lakini fedha zinaelekezwa kwenye matumizi mengine ambayo hayawagusi moja kwa moja.

Vyanzo vya makusanyo ya kodi viko vingi na kama kila mwananchi angewajibika kuilipa nchi yetu ingekuwa mbali kimaendeleo.

Kwa nchi ambazo zimepiga hatua katika maendeleo, mengi yametokana na kodi zinazokusanywa na serikali.

Wananchi pia wanaelewa umuhimu wa kulipa kodi kwasababu wanaona faida zake katika kuwahudumia kwenye sekta mbalimbali.

Udanganyifu katika ulipaji kodi unarudisha maendeleo na kuifanya serikali kubeba mzigo mkubwa kutekeleza baadhi ya miradi kwa kutegemea ufadhili au mikopo kutoka kwenye nchi zilizoendelea.

Baadhi ya wafanyabiashara hudiriki kufanya udanganyifu kwenye ulipaji kodi kwa kuandika risiti zisizo za uhalisia na bidhaa walizomuuzia mteja.

Uaminifu kwa pande zote za ulipaji na ukusanyaji ni jambo muhimu sana ili kufikia hatua zilizofikiwa na nchi nyingine duniani zilizoendelea.

Wakati mwingine uaminifu unakosekana kutokana na walipa kodi kuona fedha zao zinatumika vibaya kinyume na makusudio.

Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa akihamasisha wananchi kulipa kodi ili nchi iweze kusonga mbele na kukamilisha miradi ambayo imekwama kwa kukosa fedha.

Amekuwa akisisitiza kuwa ili nchi itekeleze miradi ya maendeleo wananchi hawana budi kulipa kodi zinazowekwa na serikali haijalishi ni ndogo au kubwa ili mradi iwe halali.

Tozo ndogo ndogo pia husaidia kwenye mapato na kujenga barabara, madaraja, shule na mambo mengine,kwa sababu hakuna serikali inayoendeshwa kwa pesa nyingine zozote isipokuwa pesa za kodi za wananchi wake.

Hata hivyo, miradi hiyo pia itunzwe ili iweze kudumu na kunufaisha vizazi vijavyo.

Lakini, kuna baadhi ya wananchi hudiriki kuharibu miradi hiyo kwa makusudi na kusababisha hasara ya kuitengeneza tena badala ya kujenga miradi mingine.

Kuna ambao wana tabia ya kuchimba na kulima pembezoni mwa barabara na kusababisha mmomonyoko wa udongo na kuharibu miundombinu hiyo.

Kilometa moja tu ya barabara ni sawa na kujenga vituo vitatu vya afya vya kata pamoja na kuweka vifaa tiba ndani.

Kuna baadhi ya wanaohujumu miradi hiyo kwa kung’oa vyuma vya kingo vilizowekwa kwenye madaraja na kwenda kutengeneza vifaa mbalimbali.

Ukiangalia gharama iliyotumika kutengeneza kingo hizo na vifaa vinavyotenezwa ni hasara kubwa. Wananchi hawafahamu sio serikali pekee inayoathirika bali hata wewe ambaye unalipa kodi.

Mara ngapi wananchi wanalalamika tozo zinazokatwa kwenye miamala ya simu, kama miundombinu itaendelea kuharibiwa hakuna shaka kuwa unafuu wa tozo hautakuwapo. 

Ni muhimu kila mwananchi kuona uchungu na kuwa mlinzi wa mwenzake ili miradi inayojengwa iendelee kudumu na mingine ijengwe kwa lengo la kuleta maendeleo makubwa.