Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis ameyasisitiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuzingatia malengo, mipango, mikakati na vipaumbele vya Taifa katika utekelezaji wa miradi.
Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo kwa Wasajili wasaidizi wa NGOs na Wajumbe wa Baraza la Taifa la NGOs (NaCONGO) Septemba 05, 2024 jijini Dodoma.
Amesema utekelezaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali unapaswa kuzingatia sio tu sheria, kanuni na miongozo ya uratibu wa Mashirika hayo, bali na matakwa ya sheria nyingine za nchi kama ilivyoainisha katika Kifungu cha 21(a) cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Sura ya 56 ya Sheria za Tanzania.
"Ikumbukwe kwamba, uzingatiaji wa misingi ya sheria, kanuni na miongozo wakati wa utekelezaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ndio msingi wa utambuzi wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika nyanja mbalimbali na Taifa kwa ujumla," amesema Naibu Waziri Mwanaidi
Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2024 linatarajiwa kuhitimishwa Septemba 06, 2024 jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED