Mama na mwanawe wauawa kinyama na watu wasiojulikana

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:50 AM Sep 07 2024
Waombolezaji.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waombolezaji.

MAMA na mtoto wake wa kike, wameuawa baada ya kufanyiwa vitendo vya ukatili na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana katika mtaa wa Muungano, Kata ya Mkonze, jijini hapa.

Waliouawa ni Mwamvita Mwakibasi (33) na binti yake Salma Ramadhani (13), mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Mkonze, Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, dada wa marehemu, Pendo Mwakibasi, alisema alipigiwa simu na mama yao mzazi anayeishi jijini Mbeya, usiku wa kuamkia jana majira ya saa 8:00 kwamba mdogo wake amevamiwa nyumbani kwake.

“Alinipigia simu kwamba nenda ninasikia huko mdogo wako amevamiwa na hiyo simu alipigiwa na mjukuu wake ambaye anakaa hapa aliyelala chumba kingine ana miaka kama 14,” alisema.

Alisema alipofika alimkuta mdogo wake huyo pamoja na mtoto wake wakiwa katika hali mbaya wakitokwa damu sehemu mbalimbali za miili wakiwa hawawezi kuzungumza. 

 “Nilikuta mmoja kitandani na mwingine yuko chini damu zimetapakaa kitandani mabongemabonge, nikasema kuna usalama kweli, nikaita majirani wakaja, tukamchukua na kumpeleka hospitalini,” alisema.

Alisema wakati tukio hilo likifanyika mdogo wake alikuwa amelala kitandani na watoto wake wawili wa kike mmoja mdogo, ambaye aliamka usiku na kutaka kwenda msalani na alipojaribu kumwamsha mama yake ndipo alipoona damu zimetakapaa mwilini.

“Ikabidi amwamshe kaka yake aliyekuwa chumba kingine ndio kutafuta simu ya mama yake hakuiona, ikabidi ampigie bibi yake ambaye ndiyo namba ameishika kichwani, ambaye ndiye mama yangu aliyeko Mbeya na yeye akanipigia,” alisema.

Alisema alimkuta mdogo wake akiwa amelala hajiwezi ametapaa damu sehemu mbalimbali za mwili wake na mtoto akiwa anakoroma aliita majirani na kuwapeleka hospitalini.

“Sijui nini kimemkuta katika hali hiyo na jana (juzi) saa 11:00 jioni nilikuwa na Mwamvita na saa 12:00 huyu binti Salma nilikuwa naye,” alisema.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Dodoma, Daniel Dendarugaho, amewataka wananchi kuwa watulivu wakati wakiendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, alipotafutwa alisema yupo nje ya kituo, lakini amelisikia na akifika ofisini atatoa taarifa.

Hivi karibuni, matukio ya mauaji katika mkoa wa Dodoma yamekuwa yakitokea mara kwa mara na ndani ya wiki hii kumeripotiwa tukio la baba kumnajisi mtoto wake wa miezi sita na kumsabishia kifo  lililotokea katika mtaa wa Mbuyuni.