WATU 12 wamefariki dunia na wengine 36 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakitumia kusafiria kutoka Mbeya kwenda Tabora kuacha njia na kugonga gema kisha kupinduka.
Hiyo ni ajali ya pili ndani ya wiki moja baada ya ile iliyotokea mwanzoni mwa wiki wilayani Mbarali na kusababisha vifo vya watu tisa. Kwa ujumla, ajali hizo mbili zimeua zaidi ya watu 20 mkoani Mbeya ndani ya wiki moja.
Ajali hiyo ambayo ilitokea jana asubuhi katika kijiji cha Lwanjilo, wilayani Mbeya, ilihusisha basi la kampuni ya AN CLASSIC lenye namba za Usajili T 282 CXT.
Wakati ajali hiyo ikitokea, inadaiwa basi hilo lilikuwa na abiria kati ya 50 na 60 na kidhibiti mwendo kilikuwa kimezimwa kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo ambao walishiriki katika uokoaji, walisema basi hilo lilikuwa katika mwendokasi hali iliyosababisha dereva ashindwe kulimudu eneo hilo ambalo lina kona kali.
Balozi wa Kitongoji cha Nsalaga mahali ilipotokea ajali hiyo, Isaka Mbuba, alisema alishuhudia basi hilo likianguka wakati alipokuwa katika harakati za kuwatangazia wananchi wake kuhudhuria mkutano wa kitongoji.
Alisema aliliona gari hilo likiwa kwenye mwendokasi wakati anasalimiana na mmoja wa wananchi wake na muda mfupi akasikia kishindo na alipogeuka aliliona limepinduka huku abiria wakipiga kelele za kuomba msaada.
Mbuba alisema aliposogea eneo la tukio alikuta watu wengi wameumia na wengine wakiwa wameminywa na gari chini, ndipo alipompigia simu mwenyekiti wa kijiji kumjulisha.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi (ACP) Wilbert Siwa, alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo ambaye alikuwa anaendesha kwa mwendokasi.
Alisema dereva alishindwa kulimudu gari katika eneo hilo kutokana na kuwa na kona kali ambayo ilistahili apunguze mwendo na hivyo akaenda kugonga gema na kisha gari kupinduka.
Kamanda Siwa alisema baadhi ya abiria wamefariki dunia papo hapo na wengine walipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Chalangwa na Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
“Bahati mbaya ni kwamba hata dereva mwenyewe amefariki dunia, baadhi ya miili imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Chalangwa na mingine ipo hospitali ya wilaya,” alisema.
Mmoja wa majeruhi waliolazwa katika Kituo cha Afya Chalangwa, Hamadi Mazinge, alisema alikuwa anatoka Mbeya kwenda nyumbani kwao, Lupa Tingatinga, wilayani Chunya.
Alisema tangu wakati wanatoka Mbeya, dereva alikuwa anaendesha kwa mwendokasi na kwamba kuna wakati walimtaka apunguze, lakini aliendelea kuendesha hivyo hadi buti kufunguka na mizigo kuanguka.
“Baada ya mizigo kuanguka alisimamisha gari na tukaipakia upya, wakati tunapakia mabasi mengine yalitupita ndipo dereva akatuambia tupande haraka tuondoke. Kwa hiyo alikuwa anakimbiza ili tuyakute mabasi yaliyokuwa yametupita. Hatukuelewa kilichotokea tukajikuta tu tupo chini,” alisema Mazinge.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, ambaye alifika eneo la ajali, alisema baada ya uchunguzi walibaini kuwa kidhibiti mwendo cha basi hilo kilikuwa kimezimwa kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Homera aliagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa ardhini (LATRA) kufuatilia mabasi yote na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa mabasi watakaobainika kuchezea mfumo wa vidhibiti mwendo hivyo.
Pia aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani hapa kuweka vibao vya tahadhari katika maeneo yote ya miteremko na kona kali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED