MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amemtaka aliyekuwa mwanachama wa chama hicho, Peter Msigwa, kumlipa fidia ya Sh. bilioni tano ndani ya siku tano na kumwomba radhi.
Aidha, amesema iwapo Msigwa akishindwa kufanya hivyo atamburuza mahakamani Jumanne ijayo.
Pia Msigwa anatakiwa ndani ya siku hizo awe amemwomba radhi Mbowe kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwamo katika magazeti ambayo yanapatikana nchi nzima.
Taarifa hiyo ya mahitaji (demand notice) imetolewa na jopo la mawakili wa Mbowe, Hekima Mwasipu, John Mallya, Simon Mrutu na Dickson Matata, kwa madai kwamba Msigwa amemchafua mteja wao.
Akizungumza jana kwa njia ya simu, Wakili Mwasipu alisema Msigwa anatakiwa kuyakamilisha hayo ndani ya siku tano tangu alipopokea taarifa hiyo, Septemba 4, mwaka huu.
"Anatakiwa kumlipa mteja wetu fidia ya Sh. bilioni tano pamoja na kumwomba msamaha hadharani kupitia vyombo vya habari, akishindwa kufanya hivi, Jumanne tunaingia mahakamani," alisema Wakili Mwasipu.
Wakili Mwasipu alisema fedha hizo ni kama adhabu maalum ya kuharibu taswira ya mteja wao kwa kumchafua.
Msigwa ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia taarifa ya jopo hilo zimesema anatakiwa kufanya hivyo, kutokana na tuhuma za uongo alizozitoa dhidi ya Mbowe.
Inadaiwa kuwa taarifa hizo ziliharibu taswira yake ya kisiasa na kifamilia katika jamii na pia, inadaiwa katika taarifa hiyo Msigwa anamtuhumu Mbowe kuanzisha 'Mbowe Foundation' na kutumia helkopta kuzunguka nchini.
Taarifa hiyo imenukuu baadhi ya maneno ya Msigwa aliyoyatoa dhidi ya Mbowe kuwa: "Mheshimiwa Mbowe ana Foundation (taasisi) hiyo si siri anayo na hiyo Mbowe Foundation ndiyo ‘actually’ ina run (endesha) chama."
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED