Agizo kuhusu ukaguzi wa mara kwa mara wa magari utekelezwe

Nipashe
Published at 12:48 PM Aug 29 2024
Usalama Barabarani.
Picha;Mtandao
Usalama Barabarani.

MAADHIMISHO ya kilele cha Wiki ya Usalama Barabarani yalifanyika juzi jijini Dodoma huku Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, akiwa mgeni rasmi. Shughuli mbalimbali zilifanyika katika maadhimisho hayo yakiwamo maandamano ya vyombo vya moto na taarifa mbalimbali pamoja na takwimu za ajali za barabarani ambazo zimeonekana kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Kuhusu ajali za barabarani, kwa mwaka 2023 ajali za barabarani zilikuwa 1,733 zilizosababisha vifo vya watu 1,647 wakati zilizotokana na pikipiki katika kipindi hicho zilikuwa 435 zilizosababisha vifo 332 ikilinganishwa na ajali 376 zilizosababisha vifo 332. 

Kwa mujibu wa takwimu hizo, ajali za barabarani zitokanazo na magari na pikipiki, zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka na kugharimu maisha ya mamia ya Watanzania huku wengine wakiachwa na ulemavu wa kudumu. 

Sababu kubwa ambazo zimekuwa zikitajwa kuwa chanzo cha tatizo hilo ni ubovu wa magari na uzembe wa madereva,   pia rushwa kwa baadhi ya askari na maofisa wa usalama barabarani imekuwa ikitajwa kwamba ni chanzo kimojawapo. 

Kutokana na takwimu hizo, Dk. Mpango alitoa maagizo kadhaa katika kudhibiti ajali hizo ikiwamo kufanyika kwa ukaguzi wa mara kwa mara wa magari. Aliweka bayana kwamba mfumo wa sasa wa ukaguzi wa magari  unaofanyika mara moja kila mwaka, tena wakati wa Wiki ya Nenda kwa Usalama, umepitwa na wakati. Kutokana na ukweli huo, Dk. Mpango aliagiza ukaguzi ufanyike angalau mara nne kila mwaka, kwa maana ya kila baada ya miezi mitatu. 

Sambamba na Dk. Mpango aliagiza udhibiti wa magari yanayobeba wanafunzi, mengi yakiwa ya shule binafsi ambayo alisema hayana ubora unaostahili ndiyo maana yamekuwa yakisababisha ajali na wanafunzi, yakiwamo mawili mkoani Arusha ambayo yaligharimu maisha ya wanafunzi. 

Pamoja na maagizo hayo yote ikiwamo matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kudhibiti ajali za barabarani, suala la ukaguzi wa magari mara kwa mara tena kila robo mwaka ni mwafaka. Hatua hiyo ni ya kuungwa mkono, hivyo inapaswa kutekelezwa na vyombo vinavyohusika vikiwamo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA) na jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani. 

Kama wahenga wasemavyo kisu kimegonga mfupa, ukaguzi wa magari na vyombo vingine vya moto mara kwa mara, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikidaiwa kuwa zinatokana na ubovu wa magari. Haiingii akilini kuona vyombo vya moto ambavyo vinabeba dhamana kubwa ya maisha ya wanadamu vinafanyiwa ukaguzi mara moja kwa mwaka. 

Utekelezaji wa suala hili uko wazi na wala hauhitaji kuwapo mijadala kwa mustakabali wa maisha ya Watanzania kwa kuwa utawezesha kulinda nguvu kazi ya taifa ambayo imekuwa ikiteketea kila uchao kwa ajili za magari. Katika suala hili, hakuna kuoneana haya wala huruma kwa sababu kufanya hivyo kutasababisha Watanzania waendelee kutoa machozi kwa kupoteza ndugu zao ambao huangamia kutokana na ajali za barabarani. 

Ni kweli kwamba magari mengi hasa mabasi yanayosafirisha abiria ndani ya miji na kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine ni mabovu kiasi kwamba yanasababisha abiria kuwa na wasiwasi kutokana na hali yalivyo. Ni imani kwamba iwapo ukaguzi utafanyika, kuna uwezekano mkubwa wa magari mabovu na yasiyokidhi viwango yakawekwa kando katika kutoa huduma za usafiri kwa abiria.