Vijana mkitumia ubunifu, mitandao kijamii mnatoka

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 11:22 AM Sep 04 2024
Vijana mkitumia ubunifu, mitandao kijamii mnatoka
Picha: Mtandao
Vijana mkitumia ubunifu, mitandao kijamii mnatoka

WAJASIRIAMALI waliofanikiwa zaidi wanaooneka zama hizi wanaelezwa kuwa, walianza safari zao katika umri mdogo, wote wana njia na mbinu tofauti zilizowafikisha kwenye mafanikio wanayoyaona sasa.

Baadhi ya vijana wanaoelekea kuwa mamilionea ni pamoja na  Fahad Awadh mwenye kiwanda cha kuchakata korosho Zanzibar wengine ni Idris Sultan aliyekuwa mshindi wa shindano la Big Brother Africa 2014 na pia wapo wengine kama Brigitha Faustin na Rahma Baju.

Baadhi ya vijana hawa wanaripotiwa na Jarida la Forbes la Marekani kuwa wana nafasi ya kuwa mamilionea wa Tanzania.

Vijana hao wanaonesha uwezo wa kuunda mazingira ya kibiashara  kutokana na juhudi na ubunifu, yote yakijulikana  nje na ndani  ya nchi  pia wakifanikishwa na teknolojia na mbinu  za kisasa.

Wengine pamoja na kujiajiri wanawapa fursa mbalimbali vijana wenzao kwa kuwaajiri na kuleta mafanikio katika umri mdogo wa wadau wanaoshirikiana nao.  

Ni wakati wa vijana kuamka maana walio wengi wamekuwa wakilalama kuhusu changamoto ya ajira na kukosa kazi na kelele za maisha  magumu yanayowakabili.

Vijana ambao ni kundi kubwa, idadi yao inatajwa katika Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 kuwa ni zaidi ya asilimia 65 wanahitaji juhudi binafsi na za wadau ili kubadilisha maisha yao kupitia biashara na uwekezaji.

Pia vijana hawa, licha ya kwamba wanataka kuwapo na mapinduzi ya mfumo wa elimu yatakayowahakikishia mitaala inayowaandaa  kwa kuwapa elimu itakayowawezesha kushiriki kikamilifu na kuwa washindani kwenye soko la ajira ni jambo ambalo linawezekana lakini siyo suluhu ya kila mmoja.

Takwimu zimethibitisha hayo kwa kuainisha kuwa, idadi ya ajira zinazopatikana zimezidiwa na wingi wa vijana wanaoingia rasmi kwenye soko la kazi wanaofikisha umri wa kujiajiri au kuajiriwa pamoja na wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu.

Teknolojia ni moja ya mambo yanayoweza kuwasaidia vijana kujikwamua na  kulia na kulalamikia  ukosefu wa  ajira,  simu janja ni fursa kubwa ya kukuza biashara kwa kutumia mitandao ya kibiashara na ya kijamii kutangaza bidhaa zao kwa wateja wa nje na ndani.

Pia, kwenye mitandao ya kijamii na kibiashara, wateja wanavutiwa kwa  kuona  bidhaa  na kupata mawasiliano kwa urahisi jambo linalohitaji pia uaminifu.

Njia hii huenda italeta unafuu na tija katika biashara zao badala ya kuzitumia simu kwenye mambo yasiyokuwa na faida, watumie simu kujijenga kimaisha ili wajikwamue kimaisha na kuondokana na umaskini.

Kupitia teknolojia  kijana ataweza kulipa kodi na kujipatia kipato. Kwa mfano, kutangaza kwenye instagram atatangaza biashara  kwa kuchapisha mambo mbalimbali kuanzia mavazi, mazao ya shamba, mifugo na maua ambayo yatajulikana kwa watu na kuvutia wateja mbalimbali.

Hivyo, kupitia mitandao ya kijamii na ya kibiashara anaweza kutanua wigo wa biashara na kuongeza kipato chake na kukuza uchumii wa nchi,  kwa sasa ndiyo njia rahisi ya kumfanya kijana kuwa na wateja wengi na kufanya biashara kwenda kwa haraka tofauti na awali.

Vilevile, kupitia teknolojia vijana wanapata wigo mpana wa kutambulisha biashara, hususani kwa mataifa mengine kwa sababu teknolojia imewasogeza watu  karibu kimawasiliano.

Hivyo, hii inaonesha ni kwa kiasi gani teknolojia itafanya vijana wajasiriamali kupiga hatua ya bidhaa wanazojihusisha nazo kwani soko ni kubwa na kuwapata wateja wapya kila wakati inawezekana kupitia  simu janja.

Ni wakati wa vijana kutumia fursa hii ili kukuza soko la biashara zao ambazo kwanza ni lazima wazisajili, watumie taasisi za kuhakiki ubora na usalama kama  Shirika la Viwango (TBS)  na Mamlaka ya Vifaa Tiba na  Dawa (TMD).

Hivyo basi, vijana wajaribu kujiajiri kupitia biashara mfano, kuuza mboga zinazozalishwa kwa kilimo hai (kisicho na  kemikali), kutengeneza bidhaa za kitamaduni na kiasili kutoka makabila mbalimbali kama vyombo vya kulia, mapambo ya kuchonga, kuchora  na kusuka.

Kadhalika kuandaa migahawa yenye vyakula vya Kiafrika na Kitanzania halisi, badala ya kutegemea chips na mayai, pilau, chapati na biriani ambavyo si asili ya Mtanzania.

Ionekane migahawa ya makande, mtori, kisamvu, tembere, perege, ugali wa muhogo na mtama vikiandaliwa kwa ubora, weledi na kuvutia watalii na Watanzania  . Yote hayo, yanaanza na ubunifu na kutumia teknolojia.