Mabaya haya yanayosambaa katika jamii, tuhoji mara mbili nafsi zetu

By Tuntule Swebe , Nipashe
Published at 07:16 AM Aug 30 2024
Tunguli.
Picha:Mtandao
Tunguli.

NI dhima potofu zimetanda, kuwapa matatizo wengine wakiamini watanufaika kwa kipato kidogo watakapotenda hivyo na wapo wanaotenda mabaya hayo kwa maslahi yao.

Imekuwa tabia sasa watu wanadhuru wengine, katika imani kwamba wanapotenda mauaji na madhara mengine, atanufaika kwa kuuza viungo vya mwili wa binadamu, bila kufikiri kuwa kitendo hicho ni kinyume cha haki za binadamu. 

Ni vyema wenye mawazo haya potofu, wakaziyeyusha fikra  hizo walizozigandisha, wakiamini mauaji na ukatili unatokea ni njia sahihi ya kuwafikisha uliko utajiri. 

Kwa uhalisia, ukweli ni kujikita na shughuli zitakazowanufaisha kama kilimo,ufugaji na ubunifu wa biashara tofauti. 

Maisha kanuni yake, hayana njia za mkato kama wengine wanavyodhani, wakatili hao dhidi ya uhai wa wenzao, wanaofanya mauaji ya wengine kuwakata viungo vya mwili, wakiwajumuisha watoto, dada na mama zao.  

Tuamke huku tukitanguliza hofu ya Mungu, huku sote wenye taarifa sahihi ya unyama huo tutoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, ambalo liko macho kufanya kazi usiku na mchana kuyakabili hayo. 

Jambo la kushangaza ni pale tunasikia na kuona wazazi wengine wanashiriki kuua watoto wao. Tunatakiwa kujua kwamba, hao ni tegemeo la taifa leo na kesho. 

Nakumbuka mnamo Juni 18 mwaka huu Jeshi la Polisi lilitangaza kumshikilia baba wa mtoto, pamoja na wenzake  kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wa miaka miwili na nusu.  

Inatisha na kuumiza kwamba maisha hayana njia ya mkato, kwani zipo shughuli nyingi zinazoweza kuleta maendeleo na kuingiza  manufaa halali, daima maisha hufanikishwa kwa kujituma. 

Kuna wanaotenda mauaji, kwa sababu ya imani potofu na madai ya ‘kuepusha mikosi katika familia au koo zao’, pasipo kuangalia upande wa pili mchafu zaidi kusigina haki za binadamu. 

Siku zote kwenye jamii, tukiepuka ramli chonganishi zinazoharibu misingi ya familia na ukoo, ndio mwanzo wa madai ya viungo vya mwili wa binadamu. 

Ni wakati wa kuamka kutatua matatizo yetu na sio kuyaongeza. Daima mtu unaweza kuingia katika tabu na kupata ukiwa kwa maovu hayo, huku wengine wao wakifanya mauaji, kwa kuamini kua kuna soko la namna hiyo na wamemeza sumu  zinazosababisha ufinyu wa fikra. 

Sisi kama jamii jambo hili ni letu sote, hivyo inatupasa kushirikiana na Polisi kuwafichua watu wanaofanya matukio hayo. 

Kwani, matukio haya ni chanzo cha kumomonyoka kwa maaadili ya vijana na chipukizi, kwa sababu kundi hilo linapokuwa linayaona hayo, wanatamani kuiga, ili waweze kurahisisha maisha. 

Nakumbuka simulizi ya kupotea watu nchini Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imesema inaendelea kufanya chunguzi maalum za matukio hayo kwa lengo la kubaini, pamoja na mambo mengine chanzo na wahusika ili kutoa mapendekezo stahiki. 

Ilikuwa Agosti 22, Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, akawaambia waandishi wa habari kuhusu matukio hayo na kubainisha mikoa inayohusishwa na uchunguzi. 

"Uchunguzi huo unaoendelea kwa sasa unahusisha mikoa ifuatayo Dar es Salaam, Singida, Mara, Simiyu,Shinyanga, Mwanza, Kagera, Geita, Kigoma, Tanga, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Arusha, Ruvuma na Rukwa. 

‘Hatua hii ni mwendelezo wa uchunguzi zinazohusu matukio ya kupotea kwa watu ambayo THBUB imekuwa ikiyafanyia kazi katika nyakati tofauti na taarifa zake kufikishwa katika vyombo vinavyohusika," anasema.

 Mwaimu anasema kuwa, katika kufanikisha lengo la  taarifa  iliyotolewa  Julai 19, mwaka huu, ikifafanua kazi zilizotekelezwa na THBUB  katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024, hasa eneo la uchunguzi wa malalamiko ya wananchi kuhusu uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji misingi ya utawala bora. 

THBUB ilikuwa imekwishafanya hatua mbalimbali ikiwamo uchambuzi wa matukio hayo kwa maana ya sehemu yalikotokea na watu waliokuwa wanadaiwa.