Mnyika asisitiza wananchi kushiriki uchaguzi wa mitaa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:18 AM Sep 07 2024
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika.
Picha: Mtandao
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kujipanga ipasavyo kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuongoza vijiji, vitongoji na mitaa nchini.

Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Majengo Shimoni, Muheza mkoani Tanga, Mnyika alisema viongozi na wanachama wanapaswa kujiandaa ili washiriki na kushinda nafasi za uchaguzi huo Novemba 27 mwaka huu. 

Alisema ushindi wa nafasi hizo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, utakuwa mwanga na dira ya ushindi wa uchaguzi mkuu wa nafasi ya Urais na Wabunge na Madiwani, unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025. 

Mnyika alisema wananchi wa Muheza, wanatakiwa ifike mahali sasa kuacha uteja wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na badala yake waikatae. 

Pamoja na mambo mengine, alisema  kuwa  serikali  ya CCM imeleta ugumu wa maisha, kwa kupanda kwa  gharama za maisha kwa wananchi  hasa  kwa  bidhaa  muhimu, ikiwemo sukari.  

Alisema  serikali ya Rais Samia Suluhu imeweza kukopa fedha nyingi kuliko marais wenzake wote waliopata nchi hii na kwamba mzigo wa kulipa hilo deni watabebeshwa wananchi.  

Aliwaonya watendaji wa serikali kuacha mara moja tabia ya kuibeba CCM katika uchaguzi na kwamba CHADEMA wapo macho kuhusu hilo. 

Mnyika aliwaomba wananchi wa wilaya ya Muheza  kwa jumla kuendesha maombi  kwa Mungu ili  kuibwaga CCM ambayo imekuwa ikileta vikwazo kuwapa shida za maisha wananchi katika nchi yao yenye utajiri mwingine wa mali lakini wananchi masikini wanafaidika viongozi.  

Awali, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Kaskazini, Yosepha Komba, alisema kuna baadhi ya viongozi wa CCM wanawatuma vijana wao kuteremsha bendera za chama hicho usiku.