KATIBU WA NEC, Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa CCM,Amos Makalla, amesema kuwa pamoja na changamoto zilizopo eneo la Ngorongoro bado wana imani na Chama Cha Mapinduzi.
Aidha,wamemweleza kuwa wana imani na Rais Samia Suluhu Hassan,ambaye atatatua changamoto zao.
Kiongozi huyo aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa Karatu na viongozi wa Ngorongoro, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku sita kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM,kutatua kero za wananchi na kuhamaisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Wakazi kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27,2024 kwa wanaCCM kukichagua chama hicho.
Alisema alikuwa na kikao kizuri na madiwani,kamati ya siasa na Leigwanani ambao wamemueleza mambo mengi ambayo ni kero kwao na atayafikisha kwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Aidha, alisema viongozi hao wameeleza hakuna chama mbadala kitakachotatua kero zao zaidi ya CCM.
"Rudini waelezeni wananchi,nimepokea changamoto zenu ninakwenda kuzifanyia kazi,"alisema.
Kwa mujibu wa Makalla,CCM iko tayari kwa uchaguzi wa serikali za mitaa ikiwa na uhakika wa ushindi wa kishindo kwenye sanduku la kura,hivyo ni muhimu wanachama na wananchi wote kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Wakazi kuanzia Seotemba 11 hadi 20,mwaka huu kwa ajili ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa Novemba 27,mwaka huu.
"CCM imekuja kwenu kuwaeleza umuhimu wa uchaguzi huu,hakuna mradi utakaotekelezwa bila kuhusisha ardhi ya kitongoji,hivyo lazima wachague kwa mnyororo wa mfanano wa viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya chini ili miradi isikwame,"alisema.
""Mafanikio tuliyoyapata kwa miaka mitano yanayokana na kwamba kuanzia ngazi za vitongoji tulichagua viongozi wa CCM na kurahisisha utekelezaji wa miradi.Tunataka Ngorongoro,Karatu na Arusha iwe ya kijani,"alisema
Tunazimq zote tunawasha zote maana yake CCM ing'ae katika uchaguzi huu.Najua wapo ambao mmewachoka hawatoi taarifa za mapato na matumizi,nawahakikishia CCM itawaletea wagombea safi wasio na 'makondakando' wagombea watakaowaunganisha wananchi,watawaletea maendeleo.
Wenyeviti wa vijiji wasiosoma taarifa za mapato na matumizi,tutawaletea wanaojua kusoma taarifa hizo.Hatutaki ambao tutaanza kuwasafisha kwa madodoki na sabuni,"alisisitiza Makalla.
Kwa mujibu wa Makalla,uchaguzi huu utapeleka salamu kwa Uchaguzi Mkuu 2024,hivyo wasikiangushe chama hicho na kwamba hiyo ndio zawadi pekee kwa Rais Samia.
"Ilani yetu ndio nyenzo sahihi ya kushinda uchaguzi ulio mbele yetu.Uchaguzi wowote unashinda kwa idadi ya kura,ili tushinde tunataka asilimia 99.999 na kwamba ili kuwa na uhakika wa kura hizo ni lazima wanaCCM wawe mstari wa mbele kujiandikisha.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED