WAKATI matukio ya migogoro baina ya binadamu na wanyamapori ikiendelea kuongezeka nchini, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, imetajwa kuongoza kwa kuwa na migogoro mingi zaidi.
Hayo yamesemwa leo na Ofisa Mhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Isaac Chamba, wakati akitoa mada kuhusu namna mamlaka hiyo inavyopambana na migogoro baina ya wanyama hao na binadamu.
Alikuwa akizungumza kwenye kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari inayoendelea wilayani Bagamoyo.
Kongamano hilo linajadili mradi unaotekelezwa na serikali wa Kukabiliana na Migogoro ya Wanyamapori na Binadamu unaofadhiliwa na Wizara ya Kiuchumi ya Maendeleo kupitia Shirika la Maendeleo ya Ujerumani (GIZ).
Chamba alisema matukio ya migogoro baina ya wanyama na binadamu yalikuwa 997 mwaka 2018 yakini yamelongezeka kwa kasi hadi kufikia matukio 3,496 mwaka jana akiongeza kuwa matukio mengi yamekuwa yakihusisha uvamizi wa Tembo.
Alisema takwimu za mwaka 2023/24 zinaonyesha kuwa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida ilikuwa na matukio 410, Nachingwea matukio 312, Lindi 260, Tunduru 218, Busega 214, Rufiji 202, Bunda 158, Liwale 112 na Chamwino matukio 111.
Alisema tembo amekuwa akichangia kwa asilimia 80 kwenye migogoro hiyo akifuatiwa na simba asilimia sita, kiboko asilimia tano, kifaru asilimia nne, mamba asilimia tatu na fisi asilimia mbili.
Alitaja baadhi ya sababu za mgongano baina ya wanyamapori na wananchi ni uharibifu wa njia za asili za wanyamapori (shoroba), zilizovamiwa na wananchi kufanya makazi na shughuli za kilimo na ufugaji.
Alisema sababu nyingine ni kukosekekana kwa mpango bora wa matumizi ya ardhi ambapo baadhi ya wananchi wamejikuta wakivamia na kuishi maeneo ya hifadhi.
“Kuna wakati mifugo ya kawaida inavamia hifadhini sasa kwa mazingira ya kawaida wanyamapori hawapatani na hawa wanaofugwa kwasababu hawa wanaofugwa wengine wamefungwa kengele au kupuliziwa dawa za aina mbalimbali,” alisema na kuongeza
“Kwa hiyo wanyamapori wanapokutana na mazingira hayo ya harufu ya dawa au kelele za kengele wanaona ni kero kwao kwa hivyo wanahama maeneo yao na wanajikuta wamehamia kwenye maeneo yenye makazi ya watu na hapo ndipo migongano inaapoanza,” alisema
Alitaja sababu nyingine kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi kama kuwepo kwa ukame mkali au mafuriko kunakosababisha wanyama kuhama kutoka kwenye maeneo yao ya asili kwenda kutafuta mawindo.
“Kama mnakumbuka kwenye yale mafuriko ya Rufiji mwaka jana mazingira yale yalisababisha mamba kusambaa kutoka maeneo yao na kwenda kwenye maeneo ya wananchi na kusababisha taharuki,” alisema
Alitaja sababu nyingine inayochangia migogoro baina ya wananchi na wanyamapori ni baadhi ya wananchi kupuuza ushauri wa wataalamu kuhusu namna ya kujilinda wanapowaona wanyamapori kwenye maeneo yao.
“Kuna tukio la mwaka juzi mkoani fulani mwalimu alijipiga picha na tembo, sasa yule tembo alishikwa na hasira akamvuta akamkanyaga na kumuua sasa tusingetarajia mtu wa kiwango cha mwalimu kufanya tukio la hatari kwa kiwango hicho na kujisababishia madhara aliyopata,” alisema
Alisema pia imani potofu imekuwa ikichangia kwani baadhi ya makabila yamekuwa yakiwatumia wanyama wakali kama fisi kama chombo cha usafiri na chombo cha kufanyia mawindo kwenye maeneo yao.
“Kuna makabila baadhi ya watu wanafuga fisi kwenye makazi yao sasa hao wanyama wakati mwingine wanavamia na kuua mifugo ya wananchi wengine na kusababisha migogoro na wenye mifugo,” alisema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED