Kaulimbiu ihamasishe kujitokeza kusajiliwa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:45 PM Aug 29 2024
Mwemyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele.
Picha: Mtandao
Mwemyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele.

NOVEMBA mwishoni mwaka huu, ni kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, na baadaye 2025 ni uchaguzi mkuu wa rais, wabunge, wawakilishi na madiwani

Wakati huu ambao nchi inaelekea katika uchaguzi huo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), nayo iko mikoani ikiendelea kuboresha daftari la kudumu la wapigakura. 

INEC inafanya kazi hiyo, ikichagizwa na kaulimbiu isemayo: " Kujiandikisha kuwa mpigakura ni msingi wa uchaguzi bora", ambayo inahimiza Watanzania kutambua umuhimu wa kujiandikisha na kushiriki katika  uchaguzi.
Kwa kaulimbiu hiyo, ni wazi kuwa  tume imedhamiria kufanya mchakato wa uchaguzi kuwa bora zaidi, iwapo kila mwananchi mwenye sifa atashiriki tangu hatua ya kwanza hadi mwisho.

Katika mzunguko wa sasa unaoendelea wa kuboresha daftari hilo wapo waliojiandikisha kwa mara ya kwanza kwa kutimiza miaka 18, hivyo, watashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

Huenda kufikia uchaguzi mkuu mwakani, wakawepo wengine watakaokuwa wametimiza miaka hiyo wakati huo.

Mchakato unaoendelea sasa ni wa muhimu, kwa kuwa ndio unaohimizwa na kaulimbiu, inayohimiza kutaka kila Mtanzania mwenye sifa ajiandiakishe ili achague viongozi wa nchi.

Hivyo, kila anayejua kwamba ana sifa za kuwa mpigakura, katika uchaguzi ujao, ajitokeze ili tume imuorodheshe katika daftari la kudumu la wapigakura au iboreshe taarifa zake.

Miongoni mwa sifa zinazotajwa na tume ambazo mtu anatakiwa kuwa nazo ni uraia wa Tanzania, umri wa miaka 18 na akili timamu, Kwa kuwa kujiandikisha kuwa mpigakura ni msingi wa uchaguzi bora, Watanzania hawana budi kulitambua hilo na kulifanyia kazi.

Kwa nini? Kwa sababu wapo baadhi ya watu ambao husema hawaoni umuhimu wa kupiga kura, kwa maelezo kwamba hata wakimpigia mgombea wanayemtaka, anashinda mwingine wasiyemtaka.

Hiyo ni miongoni mwa sababu zao, lakini sidhani kwamba kususa ni sawa, kwani kususa kunamfanya mgombea asiyetakiwa kushinda kirahisi. 

Hivyo, njia nzuri ni kuendelea kupiga kura katika mazingira yoyote badala ya kususia na kuwafanya wengine kuchagua mgombea usiyemtaka.

Ninaamini elimu ya mpigakura inaendelea kutolewa wakati huu ambao tume inaboreaha daftari la kudumu la wapigakura, hivyo, tuitumie kutambua haki za kuboresha taarifa zetu  ili baadaye tushiriki katika uchaguzi.

Kitendo cha tume kuja na kaulimbiu hiyo, kinaonyesha imedhamiria kuboresha uchaguzi, hivyo, ingekuwa ni vyema kuiunga mkono kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa za kila raia.

Vilevile, tunapokwenda kuboresha taarifa zetu au kujiandikisha, ni muhimu kuepuka mambo kadhaa ambayo tume inayataja, ikiwamo mtu kutoa taarifa zake lakini za uongo.

INEC pia inasema ni makosa kutoa taarifa za uongo za mtu mwingine kwa lengo la kuandikishwa kuwa mpigakura, hivyo, hairuhusu hilo litokee.

Pia, wananchi wanatakiwa kuepuka kuomba kuandikishwa zaidi ya mara moja au kutoa tamko la uongo kuhusu kupotea au kuharibika kwa kadi ya mpigakura ama kifo.

Mwananchi pia anatakiwa kuepuka kununua au kuuza kadi ya mpigakura na kuiba ama kuharibu kadi ya mpigakura, mkazo ukiwa ni kaulimbiu ya "kujiandikisha kuwa mpigakura ni msingi wa uchaguzi bora". 
 Ninaamini hayo yakizingatiwa, lengo la tume la kuandikisha wapigakura wapya 5,586,433 litatimia, lakini pia lengo la kuboresha taarifa za wapigakura litawezesha kupata vijana na raia wengi zaidi kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia.

Kumbuka uchaguzi wa viongozi wa mchakato wa kidemokrasia ambao unampa kila raia nafasi ya kumchagua anayeamini anafaa kumuongoza.