Sababu za Mwabukusi kuibwaga TLS kortini

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:28 AM Jul 27 2024
Wakili Boniface Mwabukusi (kushoto), akisindikizwa na mawakili wenzake, baada ya kushinda kesi dhidi ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam jana.
PICHA: IMANI NATHANIEL
Wakili Boniface Mwabukusi (kushoto), akisindikizwa na mawakili wenzake, baada ya kushinda kesi dhidi ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam jana.

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imetengua uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), uliomwengua Boniface Mwabukusi kugombea urais wa chama hicho, huku ikitoa sababu mbili za kufikia uamuzi huo.

Kutokana na uamuzi huo, Mwabukusi sasa ni rukhsa kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika hivi karibuni. 

Uamuzi huo ambao umemrejesha kuwania kiti hicho, ulitolewa jana na Jaji Butamo Phillip wa mahakama hiyo, ambaye amekubali hoja mbili za mawakili wake. Hoja hizo ni haki ya kusikilizwa aliyonyimwa Mwabukusi wakati wa kuenguliwa kwake; na ya pili ni Kamati ya Rufani kukosa mamlaka ya kumwondoa kwenye kinyang’anyiro. 

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Butamo alisema: “In my opinion (kwa mtazamo wangu), nakubaliana na mawakili… sheria iko wazi kabisa, haina tafsiri mbili. Ukiangalia yale maamuzi (uamuzi  wa Kamati ya Rufani), haki yake ya kusikilizwa imekiukwa. 

“Haki ya kusikilizwa ni ya msingi. Ni  kitu ambacho huwezi kucheza nacho kwa sababu ni msimamo wa sheria. Ukitoa uamuzi bila kumsikiliza mtu ni batili hata kama ungemsikiliza na hukumu ikawa hiyo hiyo.” 

Jaji Butamo alitoa uamuzi huo kwa kuzingatia kilichofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TLS iliyompitisha Mwabukusi akieleza kuwa yaliyofanywa na Kamati ya Rufani yametendwa kinyume cha sheria kwa kuwa haina mamlaka ya kumwengua, bali ilipaswa kurejesha maoni yake kwenye kamati ya uchaguzi. 

Baada ya kumaliza kusoma hukumu hiyo, zaidi ya mawakili 30 waliokuwa wanamwakilisha Mwabukusi wakiongozwa na Jebra Kambole, waliimba nyimbo ya ‘tuna imani na Mwabukusi.’ 

Uamuzi huo unamrejesha kuwa miongoni mwa wagombea sita waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TLS kugombea nafasi hiyo Juni 24, mwaka huu. Wagombea wengine waliopitishwa kuwania urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 2, jijini Dodoma ni Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda, na Sweetbert Nkuba.  

KAULI YA MWABUKUSI 

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Mwabukusi aliishukuru mahakama kwa kutenda haki kwa kuwa aliondolewa kwenye kinyang’anyiro kwa uonevu na ubabe. Alisema akichaguliwa kuongoza chama hicho, atahakikisha mawakili wanailinda nchi kwa kutumia elimu yao. 

“Mawakili ni jeshi linalolinda taifa katika uvamizi wa makaratasi na uvamizi wa kisera na kisheria. Tuna majeshi ya polisi na ya ulinzi wa wananchi, haya yanatumia bunduki na vifaru. Sisi tunatumia kalamu na kusoma. Tunapokuwa na TLS yenye kuwajibika taifa linakuwa imara. Nchi zinavamiwa kiuchumi, ni wajibu wa TLS kuwaongoza Watanzania kujua ukweli wa kisheria, wa mikataba ya kimataifa na sera za kimataifa tunazoingia. 

“Mimi ni simba nitakayeongoza kundi la simba, siamini kama tuna kondoo…na Watanzania wataanza kusikia uzito wa TLS. Tunaposema uzito maana yake ni kwamba TLS ina wajibu kwa wananchi, wanachama, serikali, kwa utawala wa sheria na mgawanyo wa madaraka katika mihimili ya dola. TLS siyo mtazamaji katika suala la utawala bora, TLS ndiye kiungo anayeifanya nchi yetu ishamiri kiuchumi, kisiasa na kidemokrasia. 

“Naenda kuifanya TLS kuwa accountable (yenye uwajibikaji na relevant (muhimu) na kuleta umoja wa mawakili. Nitasimamia maslahi ya wanachama katika nchi hii. Lazima tuhakikishe usalama, ulinzi na stahiki kwa mawakili,” alisema. 

Mwabukusi alisema uiwapo atachaguliwa, ataondoa urasimu wa kuwapatia mawakili wapya mihuri ya kazi, ambayo amedai wanaisotea kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya kuapishwa hali inayowanyiwa kazi. 

“Nawaambia mawakili vijana, msifuge mbwa mwenye meno ya palastiki, nendeni Dodoma mkanichague ili muone tutakachoenda kukifanya. Mtu akiapishwa apewe vifaa vyake vya kazi pale pale. Na wanaofikiri mawakili ni punching bag yao tunataka tuwaonyeshe kuwa huwezi kuwa bingwa kwa kukwepa ngumi tu, kuna wakati wa kukwepa na wakati wa kupiga,” alisema. 

Mwabukusi alisema anaamini mawakili watamchagua kwa kuwa amewajibika kuzuia dhulma pale alipotakiwa kufanya hivyo. 

“Tutaonyesha taasisi inayowajibika, tutaweka vioo mpaka kwenye akaunti zetu za fedha, hakuna kuficha,” alisema. 

Aliishukuru TLS kwamba haikuunga mkono kuenguliwa kwake na kwamba uonevu aliofanyiwa ulipangwa na kutekelezwa na watu wachache kwa maslahi yao na kwamba waliomfanyia figisu atawadhibiti kwa hoja ndani ya chama. 

 “Vibaka hatutawaruhusu tena kusimamia Uchaguzi, ni dhihaka na matusi kwa mawakili,” alisema huku akibainisha kuwa wataweka mfumo madhubuti wa kiutendaji na unaowajibika ili kuwabana wajanja wanaotaka kuitumia TLS kwa maslahi binafsi. 

Mwabukusi alisema atakapochaguliwa atashirikiana na wenzake kuupitia mpango mkakati wa TLS ili kurahisisha utekelezaji wake. 

MAWAKILI WANENA

Akizungumza kwa niaba ya Mawakili waliokuwa wanamwakilisha Mwabukusi, Kambole aliishukuru mahakama kwa kuendesha shauri hilo na kulimaliza ndani ya muda. 

“Tunaishukuru Mahakama kwa kukubali hoja zetu mbili za msingi ikiwamo haki ya kusikilizwa. Mahakama imesisitiza ni haki ya msingi kwa kila binadamu na imesisitiza mamlaka zinazotoa maamuzi lazima ziwe na mamlaka kisheria,” alisema. 

“Tumepokea uamuzi wa Jaji kwamba ile rufani ambayo ilikuwa imekatwa, ambayo ilikuwa inamkosesha sifa Mwabukusi kugombea uchaguzi wa TLS imefutwa. Kwa  hiyo tunashukuru kwamba sasa anaenda kwenye sanduku la kura, anakuwa miongoni mwa wagombea,” aliongeza. 

Alisema kurejeshwa kwa Mwabukusi kwenye kinyang’anyiro kutaongeza chachu kwenye uchaguzi huo akisema mawakili wamepata mgombea waliyemtaka.

“Mawakili tumewaletea mgombea mwenye sifa ambaye wanamtaka, tukutane Dodoma wafanye uchaguzi, kura nyingi ziende kwa Mwabukusi awe rais wa chama chetu,” alisema. 

Kwa mujibu wa Kambole, kifungu cha 50 cha kanuni za TLS za mwaka 2022, Kamati ya Rufani haikuwa na nguvu kumwengua bali kuwasilisha mapendekezo yake kwenye kamati ya uchaguzi iliyokuwa imempitisha.

Wakili aliyekuwa anaiwakilisha TLS, Steven Mwakibolwa, alisema wameupokea na kuukubali uamuzi wa mahakama kwa kuwa ni wa haki.

MSINGI WA KESI

Mwabukusi alifungua shauri la maombi Mahakama Kuu akiiomba kufanya marejeo ya uamuzi wa Kamati ya Rufani ya TLS iliyomwengua kwenye orodha ya wagombea Julai 05, 2024.

Alifungua shauri hilo Julai 11, 2024 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, akidai kuwa alienguliwa kwa uonevu bila kusikilizwa. 

Kamati iliyomwengua ilidai kuwa Mwabukusi alikuwa ana doa la kimaadili kwa kuzingatia kanuni ya 13 (c) kwa sababu alishatiwa hatiani kwenye Kamati ya Maadili akapewa adhabu ya onyo.