KILA kukicha mambo yanabadilika. Kila zama na kitabu chake. Kitu ambacho wengi hawakijui ni kwamba kule uswahilini hivi sasa mambo ya kwenda ukumbini na kadi yameanza kwisha.
Hivi sasa akinamama hawaalikani kwa kadi kama ilivyokuwa miaka kadhaa nyuma. Hivi sasa mambo ni mwendo wa vijora pambe na madela tu. Wanaalikana vipi, endelea kusoma.
Imezoeleka kuwa watu wanaalikana kwa kadi ya mchango na mwaliko. Mtu anakuletea kadi kama ana sherehe yake yoyote ile iwe siku ya kuzaliwa, ubatizo, maulidi, unyago, kipaimara, komunio, au kutunzana kwa kinamama.
Halafu ile kadi inaandikwa kiasi cha mchango unaotakiwa, au wowote ule uliojaaliwa kuwa nao. Mara nyingi kadi ya mchango hufuatana na ya mwaliko kwa aliyetoa, ambapo yeyote aliyenayo anatakiwa kuionesha tu mlangoni ndipo anaporuhusiwa kuingia ukumbini.
Bila kadi hiyo huwezi kuingia kwani mlangoni unakutana na mabaunsa na sura zingine ambazo ni tofauti na ulizozoea. Uliowazoea utawakuta ndani kama ukiingia.
Mtindo huu ndiyo uliozoeleka mpaka sasa. Na huu ulianza mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, ambapo awali ilikuwa tofauti.
Zamani sherehe zote zilikuwa zinafanyika nyumbani. Mtu akiwa na sherehe yake yoyote ile kama nilivyozianisha hapo juu.
Mtu anapoalikwa moja kwa moja anakwenda nyumbani kwa aliyemualika ambako ndipo sherehe hufanyika na ilikuwa hivyo miaka yote kwa miaka hiyo kuelekea nyuma.
Hakuna aliyefanya sherehe ukumbini, badala yake kula, kunywa na muziki vyote vilifanyika kwa mhusika mwenyewe.
Kwa sasa si hivyo tena, kwani watu wameacha kufanyia sherehe hizo nyumbani, badala yake hukodi ukumbi.
Unaweza kualikwa na mtu na ukaenda kwenye sherehe yake hata nyumbani kwake hukujui. Labda uwe rafiki yake mliyeshibana. Badala yake utakwenda kwenye sherehe yake na kufurahia bila kujua hata anapoishi, ili mradi tu mnafahamiana, mfanyakazi mwenzako, au jamaa tu.
Hali hii nayo sasa naona kama inaanza kufifia taratibu na kama itaendelea huko mbele tunaweza kusema mengineyo.
Imeanza kwa akinamama. Siku hizo madela na vijora pambe ndiyo vimekuwa kama kadi ya kuikingilia ukumbini.
Mlangoni mabaunsa wanakuwa wameshaambiwa na kupewa aina ya sare zinazotakiwa huko ukumbini. Bila hivyo utaishia nje. Sare inaweza kuwa moja, mbili au hata tatu, inategemea na mwenyewe jinsi alivyoandaa.
Mwenye sherehe anakuwa anatembeza sare hizo za vijora na madera kwa mashoga zake, ndugu na jamaa. Anakuwa na mzigo wa vijora na madera akitembeza na kugawa, ama kwa pesa kamili au ahadi. Anayeshindwa mzigo unakuja kuchukuliwa kabla ya sherehe na ukitimiza, basi siku hiyo mtu anavaa kwenda ukumbini. Ukionekana tu mlangoni unaruhusiwa.
Mvaaji akishapewa na mhusika, anatakiwa kutoa kuanzia Sh 8,000, hadi 15,000 kutegemea na sherehe na ubora wa vijora.
Aliyeandaa sherehe hunufaika kwa kutembeza vijora hivyo kwa sababu anakuwa amekwenda dukani na kununua kwa pesa ndogo kidogo na yeye akija kwa wenzake anazidisha bei.
Mfano akinunua vijora 30 kwa Sh. 5,000, atavigawa na Sh 8,000, na kama akivipata kwa Sh 6,000 au 7,000, atavitembeza kwa wenzake kwa Sh 10,000, na faida itakayopatikana ndiyo ya kwake.
Pesa ya ziada anayoipata inamsaidia kupunguza kama si kumaliza kabisa gharama za uendeshaji wa sherehe.
Hivyo ndivyo kinamama wa uswahilini kwa sasa amavyofanya. Hii inaweza kusababisha hata kinababa nao wakafanya hivyo kwa kutembezeana sare za fulana au mashati.
Wanawake wa uswahilini wako sahihi kwenye hili walilovumbua? Msomaji tunaomba maoni yako na tutayachapisha kwenye toleo linalofuata wiki ijayo.
Tuma meseji 0716 350534.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED