MELI ya MV.Mwanza Hapa Kazi Tu imefanya safari ya kwanza ya majaribio ya kifundi katika Ziwa Victoria yanayotarajiwa kufanyika kwa siku tatu ili kubaini utendaji kazi wa mitambo iliyosimikwa ndani ya meli hiyo.
Majaribio hayo yalianza kwa kuhusisha wataalamu 60 kutoka ndani nan je ya nchi wakiwemo wakandarasi, wafanyakazi wa meli wakiongozwa na nahodha wao, Wahandisi wa meli, Wasambazaji wa vifaa na mitambo mbalimbali iliyosimikwa kwenye meli hiyo kutoka nchi za Marekani, China, Ujerumani na Korea.
Majalibio hayo ya kiufundi katika meli hiyo yanafanyika kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa kanda ya Ziwa na nchi jirani.
Akizungumza baada ya meli hiyo kung’oa nanga katika Bandari ya Mwanza Kusini Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL Eric Hamissi alisema safari hizo ni za majaribio ya kitaalamu kuelekea kukabidhiwa rasmi kuanza kazi.
“Tunatarajia kufanya majaribia haya kwa muda wa siku tatu kulingana na atakavyoshauri Mkandarasi Mshauri baada ya kubaini mitambo hiyo inavyofanya kazi katika ubora uliokusudiwa kabla ya kumalizia sehemu iliyobaki ili Mei 31 tukabidhiwe rasmi kama ambavyo tumekubaliana kwenye mkataba,”alifafanua.
Hamissi alisema kukamilika kwa hatua hiyo baada ya siku tatu na wataalamu kuridhika na majaribio hayo kutapandisha asilimia za utekelezaji wa mradi huo hadi asilimia 96 huku akisisitiza kuwa zoezi hilo pekee linabeba asilimia 3 huku asilimia 4 zilizobaki zinamalizika ndani ya mwezi Aprili na Mei.
Meneja Mradi Mhandisi Vitus Mapunda alisema majaribio hayo yanahusisha majaribio ya mitambo iliyofungwa ndani ya meli ili kuona ufanisi wake na ufanyaji kazi wake ili kujihakikishia usalama wa meli.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED