Neema wakulima parachichi soko la China

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:42 AM Sep 07 2024
Parachichi.
Picha: Mtandao
Parachichi.

WAKULIMA wa parachichi nchini wanatarajia kupata mafanikio makubwa kiuchumi baada ya China, taifa la pili kwa kuwa na watu wengi duniani kuidhinisha kampuni za ndani kuuza zao hilo moja kwa moja kwenye soko lake.

Wizara ya Kilimo imeiarifu rasmi taasisi kilele ya tasnia ya mboga na matunda, bingwa wa sekta hiyo, Tanzania Horticultural Association (TAHA) kuwa China imefungua milango kwa parachichi zinazozalishwa Tanzania tangu Agosti 14, mwaka huu. 

Jitihada za kufungua soko la China zilianza mwaka 2018 wakati TAHA ilipobaini ukubwa na thamani ya soko hilo na kuiandikia barua serikali kupitia Wizara ya kilimo kuiomba kufanya kila namna kupitia njia rasmi na za kidiplomasia kufungua soko hilo. 

“Tunaishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwa tulipokwenda kwao mwaka 2018, kuwataarifu kuhusu soko la China, walionesha nia na utayari wa kufanya kazi na sisi kuhakikisha kuwa tunalifikia soko hilo. Tunashukuru pia Shiririka la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa ushiriki wao katika jitihada hizi,” alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dk. Jacqueline Mkindi.

Hivi karibuni, kabla ya soko la China kufunguliwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alizungumza na wanachama wa TAHA kuwafahamisha kuwa serikali ilikuwa inafanya kazi kwa muda wa ziada kukamilisha taratibu rasmi za China kufungua soko la zao la parachichi. 

Uamuzi huo wa China unatarajiwa kuwa neema kubwa kwa wakulima wa Tanzania na wauzaji zao hilo nje, kwa sababu China ina uhitaji mkubwa wa parachichi. 

 Takwimu za Kituo cha Biashara la Kimataifa zinaonyesha China mwaka 2023 iliagiza tani 66,000 za parachichi zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 151. 

Kuongezeka kwa hamu ya Uchina ya parachichi, ambayo kwa kiasi kikubwa inasukumwa na watu wa tabaka la kati wanaojali afya zao, imebadilisha "tunda la siagi" ambalo halikuwahi kuwa maarufu hadi kuwa tunda lenye thamani kubwa katika soko la matunda nchini China. 

Ingawa Tanzania ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa parachichi barani Afrika, baada ya Afrika Kusini na Kenya, wakulima wake hawakuwahi kusafirisha zao lao katika soko la China, kutokana na kukosekana kwa mkataba wa usafi na uhifadhi wa mimea (SPS). 

Ikiwa na idadi ya watu inayozidi bilioni 1.4, China kwa sasa ni nchi ya 10 kwa uagizaji wa parachichi duniani, na hivi karibuni inatarajiwa kuwa soko kuu la Tanzania la matunda hayo, ambayo tangu jadi yamekuwa yakiuzwa Ulaya na Mashariki ya Kati. 

Wakati wa ziara ya kwanza ya Rais Samia Suluhu Hassan huko Beijing, Tanzania na China zilitia saini itifaki ya mahitaji ya usafi na uhifadhi wa mimea (SPS) ili kuwezesha parachichi zinazolimwa Tanzania kuingia katika soko kubwa la China. 

Dk. Mkindi alieleza kufurahishwa kwake na kusema kuwa kitendo cha China kufungua soko lake kitaleta manufaa makubwa kwa wakulima wa ndani na kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa rafiki hayo mawili. 

Aidha alimpongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kipekee za kidiplomasia, ambazo zilifikia kilele cha ufunguzi wa soko kubwa na lenye faida la China baada ya miaka sita ya jitihada zao kugonga mwamba. 

Kwa mujibu wa Dk. Mkindi, mpango wa Rais kusaidia kufungua soko la China unaendana na mkakati wa kitaifa wa Tanzania wa kuongeza thamani ya mauzo ya nje ya horticulture hadi kufikia dola bilioni 2 kila mwaka, kutoka dola milioni 420 za sasa. 

Mwenendo wa China wa uagizaji bidhaa unaonyesha ukuaji mkubwa katika muongo uliopita, hasa katika soko la parachichi. 

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Kituo cha Biashara cha Kimataifa, thamani ya uagizaji wa parachichi nchini China iliongezeka kwa asilimia 4,359 katika kipindi cha miaka kumi, ikiongezeka kutoka dola milioni 3.4 hadi 151 milioni mwaka 2023. Mwelekeo huo wa kupanda unaonyesha kiwango cha ukuaji cha asilimia 71.5 kwa mwaka. 

Ukuaji huo si tu unaonesha kuongezeka kwa mahitaji ya parachichi nchini Uchina lakini pia unatoa picha ya namna soko linavyopanuka na kutoa fursa kwa wakulima wa Tanzania na wasafirishaji wa parachichi kupata soko la uhakika. 

Peru iliyoko katika bara la Amerika ya Kusini, imeshikilia asilimia 76 ya soko la parachichi takwimu zikionesha mwaka 2023 pekee nchi hiyo iliuza tani 50,000 za parachichi nchini China.  

Kwa kuzingatia umbali mkubwa kati ya Amerika Kusini na Uchina, Tanzania inayo faida ya urahisi wa usafirishaji wa parachichi kwa kuwa na ndege ya moja kwa moja ambayo inaweza kuwa muhimu katika kukidhi mahitaji ya Uchina ya parachichi. 

Dk. Mkindi anaona kwamba kufunguliwa kwa soko la China kutachochea uzalishaji wa parachichi nchini Tanzania, na kuwanufaisha wakulima wadogo na wakubwa kwa ongezeko la mauzo.

 Sekta ya parachichi Tanzania iko katika nafasi nzuri ya kukua kwa kasi kati ya 2023 na 2033. 

Takwimu rasmi zinaonyesha ambapo mwaka 2023 iliuza nje ya nchi tani 26,826.3, ziliingiza mapato ya takriban dola million 73. 

Makadirio ya Kituo cha Biashara cha Kimataifa yanaonesha kuwa ifikapo mwaka wa 2033, uzalishaji wa parachichi wa Tanzania unatarajiwa kuongezeka hadi tani 393,669, na mauzo ya nje yanatarajiwa kufikia tani 236,201.5, na kuleta mapato ya dola milioni 449 kwa mwaka kama bei itabaki kama ilivyo.