NGO zaonywa mahaba binafsi elimu mpigakura

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 07:07 AM Sep 07 2024
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akisalimiana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO) yatakayopata kibali cha kutoa elimu ya mpigakura kwa ajili ya uchaguzi kuwa na uzalendo na kuzuia mahaba yao kwa vyama vya siasa.

Pia ameyataka kuwa waaminifu katika fedha wanazozipata kutoka kwa wafadhili kwa kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuondoa kero zinazowakabili watanzania.

Dk. Biteko aliyasema hayo jana jijini hapa katika kilele cha Jukwaa la Mwaka la NGO 2024 sambamba na uzinduzi wa kampeni ya kukabiliana na utapiamlo inayotekelezwa na Shirika la World Vision.

Alisema mashirika hayo yanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uzalendo wa hali ya juu na kutoa elimu kwa kuonesha umuhimu wa kupiga kura na kujizuia kuweka mahaba binafsi ya vyama katika mchakato huo.

“Ninafahamu ziko NGO zimepewa nafasi ya kutoa elimu ya mpigakura na kufanya uangalizi wa mchakato unaoendelea wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura. Nitumie fursa hii kuwaomba mwendelee kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na uzalendo wa hali ya juu, mtoe elimu ya mpigakura na kuchagua viongozi wanaofaa.

 “Yawezekana kama binadamu mna mahaba na vyama vyenu, mna mapenzi na mtu fulani, jizuieni kuweka mahaba binafsi katika mchakato huu mkubwa.

“Nyie hamwezi kugeuka kuwa adui wa serikali kwa mchango wetu katika jamii na serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zenu kuhakikisha mambo mnayoyafanya yanawanufaisha watanzania kwanza, kuwaondoa umaskini na kuboresha hali zao,” alisema.

Aliyataka mashirika hayo yasikubali fedha au mtu kuwatoa katika maadili ya mtanzania na kuleta utamaduni mpya usio wao, bali kuheshimu ili watanzania waone ni sehemu yao.

Dk. Biteko pia alisema Wizara ya Fedha iko katika mchakato wa uandaaji wa mwongozo wa ushirikiano na asasi zisizo za kiserikali utakaotambua mchango wa wao hususan katika bajeti ya serikali ambao utatambulika na utaongezeka maradufu.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alisema katika mashirika hayo 1,368, imebainika Sh. trilioni 2.6 zilipokewa na Sh. trilioni 2.4 zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Alisema sekta iliyoongoza kwa mwaka 2023 ilikuwa ni sekta ya afya, ikifuatiwa na uwezeshaji wa jamii kiuchumi na ulinzi wa jamii.

Waziri Gwajima alitaja sekta nyingine ni pamoja na uhifadhi wa mazingira, sekta ya elimu, kilimo, utawala bora, maji, masuala ya jinsia na haki za binadamu.

Alisema makundi yaliyonufaika zaidi na miradi hiyo ni wanawake ambao walifikiwa kwa takribani asilimia 47.4 na vijana walifikiwa kwa takribani asilimia 30.5.

Awali, Mkurugenzi wa World Vision Tanzania , James Nditi, alisema shirika hilo limekuja na mkakati wa kutokomeza njaa na utapiamlo utakofanyikwa kwa miaka mitatu kwa gharama ya Dola za Marekani milioni tatu (sawa na Sh. bilioni 8.1) na itawafikia wakulima milioni 1.2 ambao watanufaika na mitaji na pembejeo ili kuwa na mabadiliko chanya ya kilimo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCONGO), Jasper Makala, alitaja vikwazo vinavyopunguza ufanisi wa mashirika hayo ni kuchukuliwa kama sekta binafsi, misamaha ya kodi bado tatizo na kukosekana kwa utaratibu mahsusi wa upatikanaji wa ruzuku kutoka serikalini.