Wanachama, viongozi msiturudishe tulipotoka

Nipashe
Published at 07:12 AM Jul 20 2024
Shirikisho la soka Tanzania (TFF).
Picha: Mtandao
Shirikisho la soka Tanzania (TFF).

WIKI hii kumekuwa na matukio kadhaa kwenye upande wa soka hapa nchini ikiwa ni pamoja na usajili kwa klabu mbalimbali, lakini pia tumeshuhudia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likitoa ratiba ya michezo ya Ngao ya Jamii.

Matukio mengine ni kushuhudia klabu za Simba, Yanga na Azam FC zikienda nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi kuelekea msimu mpya wa mashindano.

Matukio haya yote yana afya kwenye soka letu hasa katika kipindi hiki ambacho Ligi yetu inatajwa kuwa moja ya ligi bora Afrika ikishika nafasi ya tano.

Tunaona juhudi za dhati kutoka kwa wasimamizi wa soka letu, Shirikisho la soka Tanzania (TFF) na viongozi wa vilabu vyetu katika kulipeleka mbele soka letu ikichagizwa na juhudi za Serikali.

Kwa kipindi cha karibuni, Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha soka la Tanzania linazidi kupaa siku hadi siku huku likichagiza maendeleo ya vilabu vyetu kwenye nyanja ya kimataifa.

Hata hivyo, juhudi hizi zote zinataka kutiwa doa na masuala ambayo tulikuwa tukiyasikia na kuyaona miaka ya nyuma wakati soka letu bado halijawa kubwa kama sasa hivi.

Vitendo vya wanachama wa klabu kwenda mahakamani na kufungua kesi si ishara nzuri katika kukuza soka letu, linarudisha nyuma juhudi za wadau wote.

Tumesikia linaloendelea kwenye klabu ya Yanga baada ya baadhi ya wanachama wachache kwenda mahakamani kupinga uongozi uliopo sasa madarakani.

Inawezekana wakawa na hoja, lakini kupeleka mahakamani masuala ya michezo tena bila kupitia kwanza kwenye vyombo sahihi kwenye soka ni kutaka kulirudisha soka letu kwenye enzi za migogoro.

Nipashe tunaamini maendeleo ya sasa kwenye vilabu vyetu inatokana na utulivu kwenye uongozi na ushirikiano uliopo baina ya viongozi na wanachama.

Kuruhusu malumbano ya aina hii ni kuliandalia anguko soka letu, tufikirie kipindi cha nyuma hali ilivyokuwa wakati wa migogoro.

Kufanya vizuri kwa klabu zetu za Simba na Yanga kwenye mashindano ya Kimataifa kunatokana na utulivu uliopo sasa kwenye klabu hizo pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na wadhamini na wawekezaji.

Wanachama lazima watambue, sehemu zenye migogoro hakuna mwekezaji au mdhamini atakayethubutu kuweka pesa zake kuisaidia timu.

Furaha wanayoipata sasa hivi mashabiki kwenye klabu zao inatokana na uwekezaji unaofanywa na wadhamini wa wawekezaji, ndio maana leo hii tunaona timu za Tanzania zikicheza hatua ya robo fainali ya mashindano ya CAF, zamani haikuwa hivi.

Lakini pia mashabiki na wanachama wafahamu, ujio wa wadhamini na wawekezaji unatokana na amani na utulivu ndani ya klabu hizo, wanapaswa kudumisha amani na utulivu huo.

Tunaomba amani na utulivu kwenye klabu zetu ili bendera ya Tanzania iendelee kupeperushwa vyema kimataifa, kama kuna tofauti zozote, basi njia sahihi zifuatwe kutatua tofauti hizo.