Msimu ujao kuna VAR, wachezaji wawe makini

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:32 AM Jul 27 2024
VAR.
Picha: Mtandao
VAR.

KWA mara ya kwanza msimu ujao Ligi Kuu Tanzania Bara itachezwa ikiwa na teknokojia ya usaidizi wa video kwa waamuzi.

Ingawa haitokuwa kwenye viwanja vyote, lakini angalau viwanja viwili au vitatu vitakuwa na teknokojia hiyo ambayo ilikuwa ikililiwa sana na wadau wa soka kutokana na mambo mbalimbali yaliyokuwa yakijitokeza kwenye ligi, hasa ndani ya uwanja.

Nikisema hivyo wengi wanakumbuka kuwa kuna baadhi ya mechi waamuzi walikuwa wakikubali mabao ambayo hayakuwa halali, yaani kuna matatizo kabla ya kufungwa.

Inawezekana mchezaji aliotea kabla ya kufunga bao, kipa amechezewa madhambi au mengine yanayofanana na hayo.

Kuna mabao ambayo yalikuwa sahihi lakini yalikataliwa na waamuzi au wasaidizi wao, hivyo kuzifanya baadhi ya timu kunufaika na mabao yasiyo halali na zingine kunyimwa.

Hii yote ni kwa sababu ya waamuzi kutokuwa makini, kuchelewa kuona matukio au kutoyaona kabisa.

Kuwepo kwa VAR kutasaidia pale kunapokuwa na utata waamuzi kwenda kuangalia marudio kwenye video na kutoa maamuzi sahihi.

Najua, waamuzi na wasaidizi wao watakaokuwa vyumbani watakuwa wakiona na kutoa maamuzi kulingana na sheria 17 za soka na wala si vinginevyo.

Nikirudi kwa wachezaji ni kwamba wakati waamuzi, viongozi na mashabiki wakifurahia uwepo wa VAR, lakini kwa upande wao inaweza kuwa faida, lakini kwa kiasi kikubwa ni hasara kwa wale ambao ni watovu wa nidhamu.

Wapo baadhi ya wachezaji ni watovu wa nidhamu na mara kwa mara wamekuwa wakiwachezea wenzao rafu zisizokuwa na maana.

Tena wapo ambao wanasubiri mwamuzi amegeuka anatazama sehemu ambayo mpira umeelekea, huku anamfanyia mwenzake madhambi, kumpiga ngwala, au hata kumtwanga kiwiko.

Matukio haya yamekuwa yakitokea sana kwa baadhi ya wachezaji wakorofi, lakini ni mara chache sana kuadhibiwa kwani wamekuwa hawaonekani au waamuzi tu wanapotezea.

Marudio ya televisheni yamekuwa yakionyesha faulo hizo za hatari kwa wachezaji, lakini mwamuzi hakuweza kuona.

Kwa sasa, kutokana na VAR, likitendeka hilo, waamuzi waliokuwa vyumbani watakuwa wakimkumbusha au kumwambia au kumwita refa ili akaangalie marudio.

Pia nimeona kuna baadhi ya matukio ambao hayarudiwi na televisheni inayoonyesha mechi, hivyo natumai VAR itakata mzizi wa fitina.

Hapa sasa ni kuwakumbusha tu wachezaji kuwa hawapo kwenye giza tena kama zamani, badala yake wajue wataonekana hata kama mwamuzi yupo mbali na tukio.

Wanatakiwa kucheza kufuatana na sheria za soka, ule usela usiokuwa na kichwa wala miguu wauache kwani utakuja kuwaumbua.

Wanaweza kuzigharimu timu zao kwa kadi zisizokuwa na kichwa wala miguu. Hebu fikiria timu inaongoza bao 1-0, halafu mchezaji anamchezea rafu mwezake akiwa hana mpira, akapewa kadi nyekundu, halafu timu pinzani ikarudisha bao au hata kupata na la pili, moja kwa moja itaonekana kuwa aliyefanya hivyo amechangia kwa kiasi kikubwa klabu kufungwa.

Ndiyo maana wenzetu Ulaya huwakata mishahara wachezaji ambao ni watovu wa nidhamu. Utashangaa mchezaji kapewa kadi nyekundu ambapo huku kwetu huwatetea sana hata kama kwa makosa ya kipuuzi kabisa, lakini wenzetu hawayataki kabisa. Wanataka kama mchezaji wamemnunua kwa pesa nyingi, basi acheze soka kwa kuutumia uwezo na kipaji alichonacho, kuwanyanyang'anya mpira kwa uwezo siyo rafu za ajabu ajabu, au kuwatimba wenzao wakati hawana mpira.

Sitaki kuwataja au kuwaorodhesha baadhi ya wachezaji kwenye Ligi Kuu ambao wana tabia ya ukorofi kwa kucheza rafu zisizo za kiungwana, lakini ujio wa VAR nadhani sasa pamoja na mambo mengine, itawadhibiti sana wakorofi na wasio na nidhamu uwanjani.