Kiharusi mtihani mgumu Muhimbili

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:10 AM Oct 17 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Mohamed Janabi
Picha: Christina Mwakangale
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Mohamed Janabi

UGONJWA wa kiharusi unazidi kuwa tishio nchini. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila imetangaza kuwa theluthi ya wagonjwa wa ubongo na mishipa ya fahamu inayowahudumia kila siku, wenye matatizo ya kupooza.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Mohamed Janabi ana lingine la ziada; asilimia 60 ya wanaolazwa kila siku katika wodi ya magonjwa yasiyoambukiza, ni wagonjwa wa kiharusi.

Prof. Janabi alitoa ufafanuzi huo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akisisitiza kuwapo ongezeko kubwa la wagonjwa wa kiharusi hospitalini huko.

Alisema kutokana na hali hiyo, hospitali imeanzisha Kitengo cha Kiharusi (Stroke Unit), akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili (2022-2024), Kitengo cha Ubongo na Mishipa ya Fahamu kimehudumia wagonjwa wa nje 10,271. Kati yao, nusu wanaugua kiharusi.

Vilevile, bingwa huyo wa maradhi ya moyo, alisema kuwa katika kipindi hicho tajwa, wagonjwa wa kifafa waliohudumiwa ni zaidi ya 334 na wanaoonwa ni walio katika umri mchanga hadi wa utu uzima.

Alisema hospitali hiyo iliona kuna umuhimu wa kuanzishwa kwa kitengo hicho; hivi sasa ni maalumu kwa ajili ya kiharusi kutokana na kasi yake. Alibainisha kuwa kati ya wagonjwa 10 wanaougua mfumo wa mishipa ya fahamu na ubongo, watano hadi sita wana kiharusi.

"Kitengo cha Ubongo na Mishipa ya Fahamu awali kilikuwa kinaona wagonjwa 50 katika kliniki, lakini baada ya kuhamia huku, wanaonwa wagonjwa 150. Utaona ukubwa wa tatizo kwa miaka miwili na waliolazwa ni wastani wa wagonjwa 2,953.

"Isivyo bahati, huu ugonjwa (kiharusi) unaingia katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) na duniani wagonjwa takribani milioni sita hufariki dunia kila mwaka," alifafanua Prof. Janabi.

Alisema serikali imeendelea kuboresha huduma za kitengo hicho, wakipatiwa fedha kutokana na mkopo wa kukabiliana na athari za UVIKO-19, nao wanatoa huduma za kibingwa na za kibobezi za kiuchunguzi na matibabu kwa wagonjwa wanaofika kwa ajili ya kupata matibabu hayo.

"Idadi kubwa ya wagonjwa wa kiharusi tunaowaona ni wanaougua presha na kisukari. Baada ya kuona tatizo ni kubwa, tumeanzisha ‘Stroke Unit’, ili kupunguza madhara ya ugonjwa huu ambayo yanahitaji huduma ya dharura.

"Magonjwa ya kiharusi huchangia asilimia kubwa kwa upande wa wagonjwa wa ndani na wagonjwa wa nje ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaolazwa kila siku katika wodi ya magonjwa yasiyoambukiza, ni wagonjwa waliopata kiharusi.

"Kiharusi kipo cha aina mbili: ‘Ischemic stroke’ (mishipa imebana) na 'hemorrhagic stroke’ (mishipa imepasuka). Sasa ukiwa na wagonjwa 10 wenye aina hii ya pili, utawapoteza saba au wanane, watapoteza maisha. Ukipata aina ya kwanza, mgonjwa akifika kwa wakati utaweza kuwaokoa wanane hadi tisa.

"Lakini mtu anakuja na kiharusi, kisukari, uzito uliopitiliza na kiharusi, maana yake tafuta sababu. Kitengo hiki kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 10 kwa wakati mmoja. Tunaweza kutoa damu ya kuyeyusha damu iliyoganda kichwani, ila tuwe wazi bei, ni kubwa, Njia kubwa, chukua kinga ukiwa na kisukari, presha, tumia dawa na pili badili mtindo wa maisha," alisema.

Katika kitengo hicho, Prof. Janabi alisema utoaji huduma hutegemea wataalamu tofauti, wakiwamo wa moyo na kwamba kwa ambao wanaugua, ni hatari kufanyiwa huduma ya ‘massage’ na badala yake, alisisitiza itumike njia ya fiziotherapi.

"Wagonjwa wetu wa kiharusi hatuwafanyii ‘massage’ badala yake ni kuwafanyia mamacheza au fiziotherapi, kwa sababu ‘massage’ hufanya misuli yao kusinyaa zaidi, ukishafanya ‘massage’, mtu atajisikia mwili kulegea na kulala, hii haimfai mwenye kiharusi," alisema Prof. Janabi.

Alisema kitengo hicho pia kinatoa huduma kwa walio na kifafa kwa watu wazima. Kwa kipindi cha takribani miaka miwili hadi sasa, wamehudumia wagonjwa wa ndani 338 katika kipindi cha Oktoba 2022 hadi Septemba 2024 na wagonjwa wa nje walikuwa 4,850.

"Lengo kuu ni katika matibabu ya kisasa hata wanaougua kifafa wataweza kutibiwa kwa kufanyiwa upasuaji na si kutegemea tiba ya vidonge pekee. Ninashauri watu wabadili mtindo wa maisha, watembee kilomita zisizopungua sita kwa siku, yaani hatua 10,000 kila siku, si lazima uende ‘gym’.

"Jamii ihimili msongo wa mawazo kwa sababu mishipa ya fahamu huathiriwa pakubwa, njia rahisi ya kukabiliana ni kufanya mazoezi, mshirikishe unayemwamini katika matatizo yako, fanya vipimo, angali mara mbili au mara moja kwa mwaka, au miaka miwili itategemeana," alishauri Prof. Janabi.

Alisema kitengo hicho pia kinahudumia wagonjwa wenye changamoto za kushindwa kutembea, magonjwa ambukizi ya mishipa ya fahamu na magonjwa yatokanayo na mifumo kinga (Autoimmune Disease).

Alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa kitengo hicho wamefanikiwa kupunguza madhara kwa wagonjwa wenye kiharusi kwa kuwa wagonjwa hao kwa sasa wanakaa hospitalini kwa muda mfupi, wanapata tiba ya magonjwa ambukizi kwa haraka na usimamizi maalumu wa mazoezi tiba.

Bingwa wa Matibabu ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu hospitalini huko, Dk. Mohamed Mnacho, alisema kiharusi kwa kiwango kikubwa kwa watoto sababu kuu ni wanaougua magonjwa ya kurithi kama vile selimundu na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo.

Alisema kwa watu wazima sababu kuu ni mbili ambayo ni presha na kisukari na wengi wanaougua ni umri kuanzia miaka 40 na kwamba wanaotumia vilevi kupitiliza, wako hatarini kupata kifafa na kiharusi kwa sababu huzalisha sumu kuathiri mfumo wa fahamu.

"Kemikali za pombe huathiri mfumo wa ubongo, ndio maana mtu hukosa uwiano wa ubongo, ikiendelea seli zitakufa, ataanza kutetemeka, kuchanganyikiwa, kusahau na kuwa chanzo cha kifafa. Kama ni lazima sana kunywa pombe, kunywa chupa moja," alionya bingwa huyo.