Yaliyojificha mlipuko wa mauaji nchini

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 11:30 AM Oct 16 2024
Yaliyojificha mlipuko wa mauaji nchini
Picha:Nipashe
Yaliyojificha mlipuko wa mauaji nchini

SIKU 33 kuanzia Septemba 1 hadi Oktoba 3, mwaka huu, kumekuwapo na mauaji kadhaa ambayo yalitokana na wivu wa mapenzi, imani za kishirikina na visasi.

Katika kipindi hicho, watu 16 waliripotiwa kuuawa katika katika mikoa ya Dodoma, Tanga, Arusha, Mara, Mwanza na Dar es Salaam, hivyo kuonesha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili. 

Nipashe imefanya tathmini ya matukio kwa kipindi hicho yakihusisha visa vya watoto sita, wanawake watano na wanaume watano kuuawa kwa kuchomwa, kuchinjwa na wengine mazingira ya kutatanisha. 

Katika mkoa wa Dodoma, mauaji ya kutisha yalihusisha watoto watatu wenye umri kati ya miaka 12 na 16 akiwamo Milcah Robert (12), mhitimu wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Chilohoni.  

Wengine ni Makiwa Abdalah (16) na Salma Ramadhan (13) ambao walichomwa moto baada ya kuuawa. Pia wamo Mwamvita Mwakibasi (33) na Fatuma Mohamed (20), walipoteza maisha kwa vitendo vya ukatili,wakichomwa moto baada ya kuuawa. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, alitaja vyanzo vya mauaji hayo kuwa ni visasi, imani za ushirikina, na wivu wa mapenzi. Alisema kutokana na mauaji hayo, watu wanane walikamatwa na wengine watatu walifikishwa mahakamani. 

WATANO TANGA 

Mkoani Tanga, watu watatu walikutwa wamechomwa moto katika msitu wa Hifadhi ya Korogwe Fuel. Watu hao ni Jonais Shao (46), mwanawe Dedan Shao (8) na Salha Hassan (18) na waliuawa baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana. 

Mchungaji Jesse Shao, mwanafamilia wa Jonais, alisema walivamiwa nyumbani kwao na kisha walikamatwa na kupelekwa msituni ambako walichomwa moto. 

Pia Saumu Ngome (19), mkazi wa kijiji cha Perani, aliuawa kikatili na mumewe, Sarah Nzuga, kwa kukatwa kichwa kwa kisu, Kamanda Mchunguzi alithibitisha kuwa chanzo cha mauaji haya ni wivu wa kimapenzi.

 WAWILI WAUAWA ARUSHA

Katika Jiji la Arusha, Johnson Josephat (39), mfanyabiashara wa vyuma chakavu, alifariki dunia akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufani ya Mount Meru. Mke wa marehemu, Nasra Bakari, alisema mwanawe alishuhudia baba yake akipigwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni maofisa wa polisi. 

Pia David Mollel, mfanyabiashara wa madini ya ujenzi, alikutwa akiwa amening'inia kwenye mti. Mwili wa Mollel uligundulika ukiwa umening’inizwa juu ya mti kwa kutumia mkanda wa suruali huku uso wake ukifunikwa na kitambaa chekundu jirani na Mlima Oldonyowas. 

Rausa Mohamed (36) mkazi wa Nyamhongolo, Mwanza, aliuawa na mume wake, Dervinus Nkabatina (46), kwa kumsukuma na kuanguka kwenye sakafu kisha kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni.

 Aidha, Phares Buberwa, mwanafunzi wa shule ya msingi mkoani Mara, aliuawa na mwalimu wake, Adrian Tinchwa, kwa tuhuma za kuiba simu. 

KIONGOZI WA CHADEMA

Kifo cha Ally Kibao, aliyekuwa mjumbe wa Sekretariati ya CHADEMA, mwili wake ulipatikana eneo la Ununio, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime, liliahidi kufanya uchunguzi wa kina kubaini waliohusika na mauaji hayo. 

 MAONI YA WANAHARAKATI 

Kutokana na mauaji hayo, mashirika mbalimbali ya haki za binadamu nchini,  yameelezea wasiwasi kuhusu ongezeko la mauaji hayo. Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) ya mwaka 2023, inayoonesha wastani wa wanawake wanaouawa kila mwezi imeongezeka hadi kufikia 53 kutoka 43 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

 Ripoti hiyo iliyozinduliwa mjini Arusha pia imeonesha kuwa  mauaji mengi ya wanawake yanafanywa na ndugu wa karibu kutokana na imani za kishirikina na wivu wa kimapenzi. 

 Utafiti wa ripoti hiyo uliofanyika katika mikoa ya Geita, Shinyanga, Mwanza, Dar es Salaam na Kilimanjaro, pamoja na mambo mengine, ulikuwa na lengo la kutathmini kwa ujumla  matokeo ya visa hivyo.

 Ofisa Mwandamizi wa Masuala ya Jinsia, Wanawake, Watoto na Watu wenye Ulemavu wa LHRC, Getrude Abene, pamoja na kusisitiza kuwapo sheria zinazolinda wanawake, anaomba  ushirikiano kutoka kwa mashirika yote yanayotetea haki za wanawake.  

 Taarifa inaonesha kuwa hadi Septemba,  2022 wanawake 2,438 wameuawa ikiwa  ni sawa na wastani wa wanawake 492 kila mwaka na wastani wa wanawake 53  wanaouawa kila mwezi. 

 Jumuiya mbalimbali za kimataifa zimepitisha sheria za kupinga vitendo hivyo, azimio la Vienna la kupinga mauaji ya wanawake na wasichana, pamoja na azimio la kimataifa la Baraza la Haki za Binadamu linazitaka nchi wanachama Tanzania ikiwamo, kufanya juhudi za kutokomeza mauaji ya wanawake.

 Mwanaharakati wa haki za wanawake nchini, Judith Singibara, anasema katika kutokomeza mauaji dhidi ya wanawake, kuna haja ya kuwashirikisha wanaume katika kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia.

 “Mapambano ya kuwalinda wanawake na aina zote za unyanyasaji yamekuwa yakisikika, wanaharakati wa haki za wanawake wanasema bado kuna maeneo mengi yanahitaji kurekebishwa, ili kumlinda mwanamke na kuna haja ya kuwashirikisha wanaume na wavulana katika kampeni za kupinga ukatili,” anasema.

 Kwa mujibu wa  Ripoti ya  Jeshi la Polisi inayohusu  Makosa  ya  Jinai  dhidi ya binadamu mwaka 2022 watu  2,464 waliuawa na mwaka 2023 ilikuwa ni 2,303 sawa na asilimia 6.5 ya visa hivyo.

 Naye Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, anasema: “Ni dhahiri kwamba kuna ongezeko la mauaji nchini na ni muhimu serikali kuchukua hatua za haraka ili kulinda haki za raia. Tunahitaji kuwa na mfumo wa sheria unaotekelezeka ili kuzuia vitendo vya ukatili na kuhamasisha jamii kutoa taarifa kwa polisi."