Wanachama PSSSF waelimishwa matumizi ya TEHAMA kupata huduma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:29 PM Oct 14 2024
 Wanachama  PSSSF waelimishwa matumizi ya TEHAMA kupata huduma
Picha:Mpigapicha Wetu
Wanachama PSSSF waelimishwa matumizi ya TEHAMA kupata huduma

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umeendelea kuwaelimisha wanachama wake kutumia simu janja na computer kupata huduma zote zonazohusiana na wanachama kupitia PSSSF Kidijitali.

Afisa Uhusiano wa PSSSF, Rehema Mkamba amesema, kwa muda wa wiki nzima ya Vijana jijini Mwanza, wameweza kuwaelimisha wanachama njia mpya ya kupata huduma, ambapo mwanachama atapakua app ya PSSSF Member Portal, na hivyo kujihudumia akiwa mahali popote, wakati wowote.

 “Tumeachana na matumizi ya karatasi, hivyo mfuko unaendelea na kampeni ya kuwaelimisha wanachama wake matumizi ya PSSSF kidigitali, ambapo anaweza kuangalia michango yake, kutuma taarifa mbalimbali, kuuliza maswali na kupata majibu lakini pia wastaafu nao wanaweza, kujihakiki.” amefafanua.
 
Wiki ya vijana Kitaifa inafikia kilele leo Oktoba 14, 2024, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwahutubia zaidi ya vijana 1,000 kutoka Bara na Visiwani walioshiriki kwa kutembelea maonesho mbalimbali lakini pia kupata uelewa wa fursa za ujasiriamali, ubunifu wa kidijitali katika kujifunza na kujiajiri sambamba na elimu ya Sera mpya ya maendeleo ya vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024.