17 mbaroni tuhuma kulima bangi

By Timothy Itembe , Nipashe
Published at 02:41 PM Oct 14 2024
Bangi.
Picha:Mtandao
Bangi.

WATU 17 wamekamatwa wilayani Tarime, mkoani Mara kwa madai ya kujihusisha na kilimo cha bangi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Ngowele, amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao jana Oktoba 13,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Meja Ngowele ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya wa Tarime amesema operesheni ya msako ilianza Septemba 24, 2024 kwa ushirikiano wa wananchi.

"Watu hawa wamekamatwa kwa kujihusisha na kilimo cha bangi katika ukanda wa mto Mara. Ekari 3,700 za mashamba ya bangi zimeteketezwa,"amefafanua.

Ameongeza kuwa kamati hiyo inalaani vitendo vya wakulima kuwapa watoto wadogo kazi katika mashamba ya bangi kwa malipo duni, akisisitiza kwamba watoto wanapaswa kuwa shuleni.

Wiki iliyopita Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), iliwaambia waandishi wa habari kuwa wamebaini wanaofadhili kilimo cha bangi ni raia wa kigeni bila kutaja nchi wanakotokea.