Wadau waeleza changamoto afya ya akili, kinamama watajwa kuathirika

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 04:56 PM Oct 14 2024
Kaimu Mganga Mkuu wa Dar es Salaam, Dk. Gunini Kamba
Picha: Mtandao
Kaimu Mganga Mkuu wa Dar es Salaam, Dk. Gunini Kamba

WADAU wa afya nchini wameweka wazi hitaji la dharura la kuchukua hatua kukabiliana na changamoto zinazoongezeka za afya ya akili zinazoathiri watu na jamii kwa ujumla.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Mganga Mkuu wa Dar es Salaam, Dk. Gunini Kamba, wakati wa matembezi ya kutembea kwa ajili ya kuadhimisha siku ya afya ya akili duniani ikiwa na kauli mbiu chini inayoeleza "Akili duniani ni afya ya Mahala pa kazi".   

Dk. Kamba alisisitiza kuwa mazingira salama na yenye afya kazini yanaweza kuwa kama vigezo vya kulinda ustawi wa akili.

Alisema shughuli za mwili za mara kwa mara zinaweza kusaidia kuzuia magonjwa yasiyoambukiza, ikiwa ni pamoja na hali za afya ya akili, akihimiza washiriki kujihusisha na mazoezi.

"Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia ongezeko la ufahamu kuhusu masuala ya afya ya akili. Hata hivyo, bado yanaeleweka vibaya na kupuuziliwa mbali, hasa katika maeneo kama yetu. Kama afisa wa afya wa mkoa, nimeona jinsi hali za afya ya akili zinavyoathiri si tu watu binafsi bali pia familia na jamii nzima. Ni wakati wetu kuweka kipaumbele afya ya akili kwa dharura sawa na afya ya mwili, tukikuza mazingira ya kusaidia ambapo kila mtu anajisikia salama kutafuta msaada," alisema Dk. Kamba.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan, Sisawo Konteh aliiwashukuru wadhamini, wadau na jamii kwa ujumla kwa kufanikisha madhimisho hayo huku akisisitiza kuendeleza umoja huo ili tatizo la afya ya akili liweze kuondoka katika maisha ya watu.

Naye Kiongozi wa mradi wa CHOICE Tanzania, Prof. Ahmed Jusaban, alisema upo umuhimu wa jamii kutambua afya mahala pa kazi ili kuongeza umakini katika utendaji kazi kwa watumishi na kuwataka wakuu wa Taasisi kutokuzingatia afya ya mwili pekee kwa wafanyakazi wao bali afya ya akili ipewe kipaumbele.

Mkurugenzi Mtendaji wa Marcus Mwemezi Foundation, Belinda Nyapili, alisema tafiti walizozifanya zimeonesha kwamba kinamama wengi wa sokoni wamekabiliwa sana na madeni ya vikoba na michezo ambayo yanawaelemea na kusababisha kupata changamoto ya afya ya akili hivyo kupitia maadhimisho hayo wameshiriki ili kutoa elimu kuhusu changamoto hiyo kwani bado uelewaa ni mdogo.

“Kwenye masuala ya afya ya akili, ueleewa ni mdogo sana na ni kutu ambacho kwa muda mrefu sana hakikuwa kinaongelewa, ni wakati sasa wa kuzungumzia masuala ya afya ya akili kwa uwazi ili kama mtu akiwa anasikia na kuwa na dalili hizo za changamoto hizo aweze kupata msaada wa haraka na kurudi katika hali yake ya kawaida”

Mkurugenzi wa  Lisa Jensen Foundation, Lisa Zagar alisema mtu mwenye shida ya afya ya akili wanamtambua kwa dalili mbalimbali ikiwemo kutofanya vitu ambavyo ulikua ukifanya vikikupa furaha, Kuwa na msongo wa mawazo na wasiwasi.