Polisi waua mfugaji kwa risasi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:55 AM Oct 14 2024
Polisi waua mfugaji kwa risasi
Picha:Mtandao
Polisi waua mfugaji kwa risasi

MKAZI wa kijiji na kata ya Mirui, wilayani Liwale, mkoani Lindi, Herman Budam (17), amefariki dunia na mwingine Mbekwa Lala (20) kujeruhiwa kwa risasi na askari polisi, baada ya kutokea kinachodaiwa "vurugu za kutaka kuchukua mifugo yao iliyokamatwa na jeshi hilo".

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, mashuhuda wa tukio hilo, wazazi na ndugu, walisema tukio hilo lilitokea Oktoba 9 mwaka huu, saa 10:30 jioni.

Mashuhuda waliojitambulisha kwa majina ya Rashid Muhutusa, Jeremia Muhatsu na Michael Jacobo, walidai kuwa siku hiyo, vijana hao wakiwa wanachunga mifugo ya baba yao Herman Muhenndi, askari polisi waliokuwa kwenye operesheni ya kuzuia na kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji walifika kijijini huko.

Walidai kwamba katika operesheni hiyo askari walikamata ng’ombe 800 waliokuwa katika maeneo yasiyo rasmi wakilishwa, hali iliyowakasirisha wafugaji hao, hivyo kukusanyika wakiwa na silaha za jadi na kukabiliana na askari hao.

"Hali hiyo ilizua vurugu kubwa kati ya wafugaji na askari waliokuwa kwenye operesheni na kusababisha kifo na majeruhi," walidai.

Walidai kwamba ndugu na jamaa wa kijana huyo wamegoma kuchukua mwili wa kijana huyo, kwa madai ya kutoridhishwa na kile walichokita "uonevu waliofanyiwa na askari polisi".

Herman  Muhenndi, baba wa kijana aliyeuawa, akizungumza kwa niaba ya wafugaji wenzake, alidai wanalimiliki eneo hilo kihalali, baada ya kuuziwa na uongozi wa serikali ya kijiji husika.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kanda ya Kusini, Daudi Kalele na ndugu wa marehemu walidai hawako tayari kuchukua mwili wa kijana wao hadi Mawaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yusuf Masauni na wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega watakapofika kijijini huko kutaja waliowatuma askari hao.

Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Goodluck Mlinga, alipoulizwa kuhusu kuwapo zoezi hilo katika eneo lake la utawala, alithibitisha kulitambua na kueleza tayari wafugaji wametengewa ekari 100,000 huko Kimambi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za ufugaji.

Hata hivyo, Mlinga alisema kuwa licha ya kuwapa ekari 100,000 kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za mifugo, baadhi yao wamekuwa wanakaidi na kulisha mifugo katika mashamba na mazao ya wakulima, hivyo kusababisha vurugu zinazozalisha mauaji kwa wananchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP John Imori, alithibitisha kuwapo tukio hilo, akidai askari walikuwa katika operesheni kuzuia na kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji, wakikamata ng’ombe 800 waliokutwa eneo lisiloruhusiwa kwa shughuli za ufugaji.

Alisema kitendo cha kukamatwa mifugo hiyo, kilisababisha kundi la wafugaji waliokuwa na silaha za jadi kujitokeza na kuanzisha vurugu  za kushambulia askari waliokuwa eneo la tukio, kwa lengo la kutaka kuchukua mifugo yao iliyokamatwa.

Kamanda huyo alisema katika vurugu hizo, mfugaji aliyemtaja kwa jina la Nekava Ghutam, mkazi wa kijiji cha Mirui, alijeruhiwa kwa risasi japo alifanikiwa kukimbia kutoka eneo la tukio.

Kamanda Imori alisema mwili wa mfugaji aliyepigwa risasi uliondolewa eneo la tukio na kupelekwa Hosptali ya Wilaya ya Liwale, kwa taratibu zingine za kisheria.