Balozi Uganda aridhishwa maendeleo mradi wa EACOP

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 02:05 PM Oct 14 2024
Balozi Uganda aridhishwa  maendeleo mradi wa EACOP
Picha: Mpigapicha Wetu
Balozi Uganda aridhishwa maendeleo mradi wa EACOP

BALOZI wa Uganda nchini Tanzania, Kanali (mstaafu) Fred Mwesigye amevutiwa na utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP), akisema kukamilika kuwa utakuza uchumi wa mataifa hayo mawili na kutoa ajira kwa wananchi wake.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa ziara ya viongozi mbalimbali kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania na Uganda kwa ajili ya kujionea maendeleo ya mradi huo katika Kijiji cha Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora, Balozi Mwesigye amesema mradi huo ni mkubwa kupata kutokea katika Afrika.

"Mradi huu utaacha alama kubwa katika mataifa haya, ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakishirikiana katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo.”

"Wameamua kutembelea katika kiwanda hicho cha Sojo kwa sababu ni eneo muhimu katika utekelezaji wa mradi huu, akimwakilisha Rais wa Uganda Yoweri Museveni ili kujionea kazi zinavyofanyika.

“Mabomba yote yanayotoka nje ya nchi yanaletwa hapa na kuwekewa koti juu ili kusaidia usafirishaji wa mafuta ghafi (mazito) yanayotoka Uganda kwenda Pwani ya Tanga na baadaye kusafirishwa nje ya nchi.

"Yatafukiwa aridhini kuanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga yakiwa na umbali wa kilomita 1443, hivyo ni eneo muhimu sana katika utekelezaji wa mradi huu,"amesema.

Akielezea kuhusu faida za utekelezaji wa mradi huu, Balozi Mwesigye amesema uchumi wa nchi hizi utakuwa kwa kiasi kikubwa kupitia tozo mbalimbali za kodi na ajira zinazotolewa kwa kampuni za ndani ya wazawa kwa ajili ya kutoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mradi na ajira zinazotolewa kwa wataalamu wazawa wakiwemo watu wasio na ujuzi wanaoishi kando kando ya bomba hili linapopita katika mikoa nane hapa nchini.

Amesema hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo ni kubwa na ya kujivunia na hii ni ishara ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa mpaka sasa.

“Nitafurahi kuwaona wabunge wa Uganda na Tanzania kwa pamoja wakitembelea pia eneo hili ambalo mabomba yote ya mradi yanafikia hapa, ili waone hatua iliyofikiwa mpaka sasa katika utekelezaji wake.

“Nilikuwa hapa Sojo miaka miwili iliyopita wakati mradi huu ukiwa katika hatua za awali na leo hii nimeshuhudia maendeleo makubwa, ikiwemo sehemu moja ya kiwanda ikianza uzalishaji ambapo mabomba yote yatakayosafirishwa kwenda sehemu mbalimbali ikiwemo Uganda,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Mafuta nchini Uganda (PAU), Ernest Rubondo amesema amefurahishwakuona maendeleo na hatua ya mradi huu yaliyofikiwa mpaka sasa.

Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali na utakuwa na faida kubwa kwa maendeleo ya nchi hizi.

Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Mafuta kutoka Mamlaka ya ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Gerald Maganga amesema wamefurahishwa na maendeleo ya mradi huo na kuona Kiwanda cha Sojo kinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.